Mtandao wataka marekebisho sheria za usalama barabarani

Waandishi wa  habari wakiwa katika mafunzo yanahusu usalama barabaran i yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa  Habari Wanawake(TAMWA)Picha na Jasmine Shamwepu.
MADHARA yanayosababishwa na ajali barabarani yemeongezeka katika miaka ya hivi karibuni licha ya kuwepo kwa jitihada za Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani. Kikosi hicho kinakadiria kuwa kwa mwaka 2015 takribani ajali 8337 zimerekodiwa na kusababisha vifo 3468 na majeruhi 9383.  Katika makala haya Mwandishi wetu Jasmine Shamwepu anafafanua jitihada zinazofanywa na wadau mbalimbali kukabili ajali hizo.

 Kwa Tanzania Bara, taarifa za Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani zinaonyesha mwaka 2016 jumla ya watu 3,256 walipoteza maisha kutokana na ajali za barabarani. Katika vifo hivyo wanaume walikuwa 2,580 na wanawake 676. Aidha majeruhi walikuwa 8,958 kati yao wanaume 6470 na wanawake ni 2488.

Taarifa zinasema vyombo vya moto vilivyoongoza katika ajali ni magari binafsi ambayo yalifikia 3,649 yakifuatiwa na pikipiki 2544.

 Taarifa za jeshi hilo pia zinaonyesha kuwa vyanzo vikubwa vya ajali ni pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara, ukosefu  wa udhibiti madhubuti wa vyombo vya usafiri pamoja na matumizi mabaya ya barabara kwa watumiaji wote hususan waenda kwa miguu, bodaboda, magari binafsi, baiskeli, mikokoteni, mifugo na magari ya mizigo na abiria.

 Asha Hamisi ni abiria anayetumia usafiri wa umma na mkazi wa eneo la Nkuhungu mjini Dodoma. Katika maoni yake anasema ajali barabarani zimeendelea kusababisha athari nyingi kiuchumi na kijamii huku maelefu ya nguvu kazi ya Taifa hususan vijana wakipata ulemavu wa kudumu na athari za kisaikolojia na umaskini.

 “Gharama za maisha zinaongezeka hata katika ngazi ya kaya na kwa upande wa Serikali kuingia gharama za kuhudumia sekta ya afya, “anafafanua Hamisi na kubainisha athari za kiuchumi kwa waathirika ambao wanashindwa kufanya kazi za kujiingizia kipato kutokana na ulemavu, vifo, ugonjwa wa kudumu kutokana na majeraha na zaidi ni kukosa msaada wa kaya ambazo zimebaki kuwa tegemezi baada ya kuondokewa na watu muhimu waliokuwa nguzo katika familia.

 Naye Prisca Daniel ambaye ni abiria wa bodaboda anasema pamoja na athari za moja kwa moja watu wengi bado hawana elimu ya usalama barabarani. “Namaanisha wote, madereva na watumiaji wengine wa barabara. Serikali ingeweka mpango wa kudumu wa kuita watu kwenye mikutano ya hadhara na kutoa semina kuhusu matumizi bora ya barabara ili kupunguza ajali.

Akizungumzia madereva wa boda boda anasema vijana wengi wanatumia pombe kwenye viroba, wamekuwa wakorofi, hawaheshimu sheria za usalama barabarani.

 Kwa upande wake dereva wa bodaboda Michael Dickson anasema madereva wengi siku hizi wanazingatia sheria lakini madereva wa malori makubwa na daladala wanawapuuza na kuwadharau “Usipokuwa makini wanakubana kwenye barabara, hata kwenye eneo la mataa wanakusogelea na kukutisha kwa honi hata kama uko kwenye eneo lako watakufuata, hii ni hatari kwetu,” anasema Dickson huku akiwashushia wanawake lawama kwa kukataa kuvaa kofia wakidai ni chafu.

 “Hata tukiwalazimisha hawataki na tukiwabeba bila kuvaa kofia ngumu tunakamatwa” analalamika na kuhoji anayekataa tutamfanyaje.

 Takwimu zinaonyesha kuwa ajali zinazotokea Tanzania kila mwaka husababisha upotevu wa asilimia 3.4 ya pato jumla la Taifa huku takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zikibainisha wazi kuwa watu milioni 1.24 hufariki kila mwaka kutokana na ajali za barabarani (WHO: 2013).

 Kwa mujibu wa takwimu ajali nyingi zinazotokea Tanzania husababishwa na makosa ya kibinadamu kwa watumiaji wa barabara. Jeshi la Polisi linakadiria kuwa asilimia 76 ya ajali zote zinazotokea barabarani husababishwa na makosa yatokanayo na uzembe wa watumiaji wa barabara huku asilimia 8 ikitokana na ubovu wa miundombinu. Aidha asilimia 16 husababishwa na ubovu wa vyombo vya moto vya usafiri vinavyotumika barabarani bila kukaguliwa au bila uangalifu.

 Kimsingi ajali nyingi zinaweza kuepukika endapo madereva na watumiaji wengine wa barabara wataheshimu na kuzingatia sheria na kanuniza usalama barabarani. Inakadiriwa kuwa endapo hatua hazitachukuliwa na watunga sera wakishirikiana na watunga sheria, ajali za barabarani zitakuwa ndio chanzo kikuu cha vifo duniani.

 SHERIA YA USALAMA BARABARANI YA 1973

 Kwa mujibu wa Sheria mama ya usalama barabarani (Sura ya 168 ya Sheria za Tanzania, Toleo la 2002), inayosimamia suala la usalama barabarani zipo sheria nyingine katika sekta ya usafirishaji pamoja na sera mbalimbali ambazo kwa namna moja au nyingine zinahusika na masuala ya usalama barabarani.

 Sheria mama (2002) inasimamia masuala ya usajili wa magari, utoaji wa leseni za udereva, matumizi ya vyombo vya usafiri barabarani pamoja na utaratibu mzima wa kutoa adhabu mbalimbali stahili zinazohusiana na makosa dhidi ya sheria hiyo. Kimsingi Sheria hiyo imejitahidi kukabiliana na changamoto za ajali zinazoongezeka siku hadi siku na kusababisha maafa makubwa ya watanzania.

 Hata hivyo utafiti uliofanyika unabainisha kuwa sheria hiyo ikibaki ilivyo bila marekebisho kadhaa, haijitoshelezi na kwamba haiwezi kumaliza tatizo sugu linalokuwa kwa kasi la ajali barabarani. Kwa hivyo utafiti unabainisha wazi kuwa sheria hiyo ina mapungufu kadha wa kadha kiasi cha kushindwa kutimiza lengo lililokusudiwa la kukabiliana na tatizo la ajali za barabarani.

 VISABABISHI (VIASHIRIA) VITANO VYA AJALI TANZANIA

 Uchambuzi wa kina wa Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 unajikita katika mwendo kasi, uvaaji wa kofia ngumu (helmet), ufungaji wa mikanda, matumizi ya kilevi na vizuizi vya watoto.

 Mwanasheria kutoka Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA) Mary Richard anazungumzia malengo ya kuanzisha mtandao wa kitaifa kuhusu masuala ya usalama barabarani na kuutumia kusisitiza utekelezaji wa sheria za usalama barabarani.

 Awali anasema sheria yenyewe imejikita katika viashiria vinne tu ambavyo hata hivyo havikupewa ufafanuzi wa kina kwa kiwango kamili kinachowezesha kudhibiti au kupunguza ajali za barabarani.

 Mtandao wa Usalama Brabarani Unafanya nini?

 Kwa mujibu wa Mwanasheria huyo wa TAWLA mtandao wa wadau kutoka taasisi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera ihusuyo usalama barabarani Tanzania ulikutana na Wabunge na waandishi wa habari na wadau wengine Januari 27, 2017 mjini Dodoma. Wabunge kutoka Kamati ya Mambo ya nje, ulinzi na usalama, Katiba na Sheria na Miundo mbinu chini ya mwenyekiti wake Balozi Adadi Rajabu (Mbunge wa Muheza) ilipokea mada zilizowasilishwa na kujadiliwa kuhusu masuala ya usalama barabarani, hali halisi ilivyo na mikakati ya kutetea marekebisho ya sheria na sera za usalama barabarani ili kupunguza kasi ya ajali nchini.

 Taasisi zinazounda Mtandao wa wadau kutoka asasi za kiraia unaotetea marekebisho ya sheria na sera ihusuyo usalama barabarani Tanzania hadi sasa ni pamoja na Tanganyika Law Society, Tanzania Child Rights Forum (TCRF), Tanzania Media Foundation (TMF), Road Safety Ambassadors, AMEND Tanzania na TABOA. Taasisi nyingine ni Safe Speed Foundation, Women Legal Aid Centre (WLAC), Tanzania Media Women Association (TAMWA), Tanzania Women Lawyer Association (TAWLA) na Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA)

Kwa upande wao wabunge walikiri kuguswa na matokeo ya ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ambayo inaonyesha watu milioni 1.25 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na ajali za barabarani na kati yao watu milioni 20 mpaka 50 hupata ulemavu kila mwaka na wengi wakiwa vijana wenye nguvu kazi ya Taifa huku nchi za Kiafrika hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara zikiathirika zaidi ikiwemo Tanzania.

 Mbunge wa Muheza Adadi Rajabu anasema wataanza kwa kutoa elimu na kutoa tahadhari kwa wananchi na madereva wanazingatia usalama barabarani na kujenga utamaduni wa kufuata sheria za usalama barabarani. “Tungependa kuona mswada wa marekebisho ya sheria hii unakuja mapema bungeni ili tuweze kuushughulikia ili kuongeza udhibiti kwa maeneo yanayosababisha ajali zinazoweza kuzuilika” anasema Rajabu.

Kutokana na hali halisi na mjadala kuhusu umuhimu wa jambo hilo wabunge waliamua kulifanyia kazi kwa kina na kuweka mikakati ya kitaifa ya kupunguza ajali na kukubali kuunda mtandao wa wabunge wanaotetea usalama barabarani huku wakiunga mkono mapendekezo yote ya wanaharakati yaliyobainishwa kwa kina kwenye viashiria vitano vya ajali ambavyo vimebainishwa kama maeneo ya vipaumbele katika marekebisho ya sheria ya usalama barabarani.

 Viashiria hivyo vya ajali ni mwendokasi, ulevi au unywaji pombe, kutokuvaa kofia ngumu (helmet), kutokufunga mikanda na zaidi kutotumia vizuio kwa watoto ambapo imebainishwa sheria ya barabarani (sura ya 168 ya mwaka 1973) ambayo inaonyesha upungufu katika kifungu cha 51(8) kinachobainisha mwendokasi usifanyike maeneo ya makazi ya watu kwa zaidi ya kilomita 50 kwa saa na kutoa fursa kwa maeneo mengine yote ambayo eti yatadhibitiwa tu kwa alama za barabarani.

 Kifungu hicho pia kinatoa fursa kwa magari yanayozidi tani 3500 kutozidisha mwendo kasi kuzidi Kilomita 80 kwa saa na kwa mujibu wa uchambuzi wa wanaharakati Sheria hiyo inatambua maeneo machache sana katika kuzuia mwendokasi, “ Kuna maeneo mengi hayajatambuliwa wazi na sheria hii kwa mfano,  imetambua baadhi tu ya magari kama vile magari ya biashara, magari yenye uzito mkubwa na yale yanayotumika kama usafiri kwa umma huku ikitambua aina (class) maalum ya barabara kwa ajili ya mwendokasi” wanasema wanaharakati hao na kusisitiza kuwa huo ni udhaifu wa kisheria unaotakiwa kudhibitiwa kwa kurekebishwa vifungu hivyo kwa vile vinatoa mwanya wa kuongezeka kwa kasi ya ajali mbaya barabarani.
,
 Badala yake wametaka sheria mpya itungwe na kutambua maeneo yote na si yale ya mjini au maeneo ya makazi, “sheria itamke wazi kuhusu maeneo ya shule, maeneo ya michezo, mbuga za wanyama nakadhalika kwa ajili ya kuzuia mwendokasi na kwamba izingatie aina zote za magari na siyo magari ya biashara, yenye uzito mkubwa na yale yatumikayo kwa usafiri wa umma pekee,” tamko hilo lilibainisha na kuongeza kuwa kwa ajili ya utekelezaji na utendaji; sheria iweke mawanda mapana ya kupunguza mwenzokasi katika sheria Kuu na sio kupitia kanuni zinazotungwa chini ya mamlaka ya waziri.  “Aidha Sheria itambue aina maalum ya barabara zilizotengwa kwa mwendokasi maalum,”tamko hilo lililowasilishwa na Mratibu wa Mradi wa Usalama Barabarani Gladness Mnuo kutoka TAMWA lilifafanua.

Comments

Tanzania

TAARIFA MBAYA KWA WAVUTAJI WA SIGARA, TUMBAKU

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

MADAI YA WAFANYAKAZI YASABABISHA VIFAA VYA UJENZI VYA KAMPUNI YA  CEYTUN KUZUIWA UWANJA WA NDEGE TABORA.