WAUMINI WA KIISLAMU WATUMIE MWEZI WA RAMADHANI KUKEMEA UHARIFU


Na Mwandishi Wetu,Pwani WAUMINI wa dini ya kiislamu waliopo katika Kata ya Kongowe Halmashauri ya Mji wa Kibaha wametakiwa kuutumia mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa kutanguliza mbele maslahi ya nchi katika kuhubiri amani pamoja na kukemea vitendo vya uharifu vinavyofanywa na baadhi ya watu. Diwani wa kata ya Kongowe Idd Kanyalu(CCM),alitoa wito huo juzi wakati akizungumza na waumini zaidi ya 200 wa msikiti wa Bamba mara baada ya kumaliza zoezi la kufuturisha lililokuwa likifanyika msikitini hapo. Kanyalu,alisema kuwa mwezi wa Ramadhani ni mwezi ambao kila muumini anapaswa kuuheshimu kwa kutenda mambo mema yanayompendeza mwenyezi Mungu hivyo ni fursa nzuri ya kuhakikisha wanaleta mabadiliko katika jamii. Alisema, wapo watu wachache ambao wamekuwa wakifanya vitendo vya uharifu vinavyopelekea uvunjifu wa amani katika nchi yetu jambo ambalo haliwezi kukubalika kwa kuwaacha watu hao waendelee . Kanyalu,alisema kuwa ni wakati muafaka kwa waumini wote wa dini ya kiislamu kuhakikisha wanautumia vyema mwezi mtukufu wa Ramadhani katika kukemea vitendo hivyo ikiwemo kuwafichua waharifu wanaojificha katika jamii. “Waumini wenzangu wa dini ya kiislamu tunapokuwa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani naomba tushirikiane katika kuhubiri amani ya nchi yetu maana bila amani tusingeweza kufanya jambo lolote hapa msikitini na pia hakuna maendeleo yanayoweza kufanyika,”alisema Kanyalu Aidha ,Kanyalu alisema kuwa zoezi la kufuturisha litaendelea kufanyika katika misikiti mingine na kwamba kwasasa tayari amefanya katika misikiti miwili iliyopo kwenye Kata yake ukiwemo wa Bamba . Hatahivyo,Kanyalu aliwataka waumini hao pamoja na wananchi wa Kata ya Kongowe kiujumla kuendelea kushirikiana kwa pamoja katika kupigania maendeleo ya Kata yao kwa kutatua changamoto zilizopo. MWISHO.

Comments

Tanzania

TAARIFA MBAYA KWA WAVUTAJI WA SIGARA, TUMBAKU

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

MADAI YA WAFANYAKAZI YASABABISHA VIFAA VYA UJENZI VYA KAMPUNI YA  CEYTUN KUZUIWA UWANJA WA NDEGE TABORA.