Ndoa ni ninyi wenyewe, siyo watu wa nje


Na Dismas Lyassa SIRI moja kubwa ya kuwa na ndoa nzuri ni wanandoa wenyewe kujitambua kuwa wao ndiyo wenye deni la kuimarisha uhusiano walionao. Ndiyo kusema kuwa kila siku katika maisha yako, unapaswa kutafuta mbinu za kufanya ili uhusiano wenu uendelee kuwa mzuri. Siku moja nilikuwa napita Sinza (Dar es Salaam), nikamsikia dada mmoja akijibizana na mwenzi wake kwenye simu; “Aah kwani wewe unataka muda huu niwe wapi? Haya basi niko chooni.” Hayakuwa majibu mazuri, kiasi dada mwingine aliyekuwa karibu, akamsihi mwenzake asizungumze vile. Watu wengi wanapenda kuwa na ndoa nzuri, lakini wao hawajui kuwafanyia mazuri wenzao. Utakuwaje na ndoa nzuri wakati kauli zako ni chafu? Jitahidi kuwa na kauli nzuri kwa mwenzi wako. Hata pale mwenziyo anapokukosea, zungumza naye kwa njia ya kuondoa kasoro, si kutukanana. Siku zote waza namna ya kuujenga uhusiano wenu. Usidhani ndoa nzuri za wenzio ni jambo linaloshindikana kwako, hapana. Ndoa haijengwi kwa matofali, bali kauli njema na matendo mema. Kumbuka hakuna mtu aliyezaliwa aje kuiimarisha ndoa yako, ni wewe mwenyewe unapaswa kufanya kazi hiyo. Anza leo kuchukua hatua kama ndoa yako ina walakini huo, utashangaa utakavyokuwa na ndoa nzuri. Katika maisha hakuna lisilowezekana. Kwanza weka lengo, kisha chukua hatua, utafanikiwa. Ni muhimu kujifunza masuala haya kwani elimu haina mwisho. Wengi wakishaingia kwenye ndoa, basi hudhani wameshamaliza kila kitu. Ni makosa makubwa, unapaswa kuendelea kutafuta mbinu mpya kila siku ili mfaidi raha za ndoa. Kuna mengi ya kujifunza: Katika ndoa kuna mengi ya kujifunza, mojawapo ni kujua mwenzi wako anapenda nini. Kwa mfano wanaume wengi wanapenda wake zao wawe na utayari katika mahusiano. Unaweza kushangaa, lakini ni ukweli. Tafiti zinaonyesha watu wasio kwenye ndoa hukutana kimwili mara nyingi zaidi kuliko walio kwenye ndoa, licha ya kuwa wanalala kitanda kimoja. Watu wakishaingia kwenye ndoa, hufanya tendo hilo kwa muda mfupi zaidi kuliko ilivyokuwa kabla hawajaoana, unajua ni kwa nini? Utayari huwa matatizoni. Sababu ziko nyingi, lakini mojawapo ni wanaume wengi kurudi majumbani wamelewa chakari, wananuka pombe na wake zao wanalazimika tu, wafanyeje. Lakini wakati wa uchumba, wanaume hao huenda kwa wapenzi wao wakiwa hawajalewa. Ndiyo ukweli Kimsingi wanandoa kila mmoja anatarajia kuona mwenzi wake anamjali na anamsikiliza. Kufanikiwa hili, lazima kutumia akili. Kuna ambao licha ya kuwa tayari kaingia kwenye ndoa, lakini kwa upumbavu, anazungumzia habari za mpenzi wa zamani. Pia kuna walio kwenye ndoa, lakini wanajali zaidi watu wengine wa nje au kuwasikiliza zaidi wazazi ambao mara kadhaa wamekuwa chanzo cha ndoa kuvunjika. Jamani hata Biblia imeandika; “Mtu atawaacha wazazi wake na kuandamana na mkewe, hao wawili watakuwa mwili mmoja.” Wengine wako katika ndoa lakini wana lundo la wapenzi nje. Hapo ndoa yako ikiyumba utamlaumu nani? Fanya jitihada kuipa uhai ndoa yako, iwe paradiso ya kweli. Kuna ambao badala ya kutamani kurudi nyumbani, wao hutamani kuchelewa, maana nyumbani hakukaliki. Yaani hakuna mapenzi, hakuna kinachovutia. Mume au mke hapendi kujifunza mambo zaidi. Ndugu yangu rekebisha ndoa yako, uishi kwa furaha. Dismas Lyassa ni mtaalam wa mahusiano, wasiliana naye kwa simu 0754 498972 au 0786 148105 MWISHO.

Comments

Tanzania

TAARIFA MBAYA KWA WAVUTAJI WA SIGARA, TUMBAKU

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

MADAI YA WAFANYAKAZI YASABABISHA VIFAA VYA UJENZI VYA KAMPUNI YA  CEYTUN KUZUIWA UWANJA WA NDEGE TABORA.