Maghembe: waandishi saidieni kuwafichua majangili


Na Yusuph Mussa, Tanga WAZIRI wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe amewataka waandishi wa habari kuwafichua kwa kutumia kalamu zao watu wanaojihusisha na ujangili. Amesema pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali za kupambana na ujangili, bado majangili wapo, na wengine ndani ya Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA), hivyo waandishi wakitumia mbinu zao watafanikisha. Aliyasema hayo jana (Julai 27) wakati anafungua warsha ya siku tatu kwa wahariri na waandishi wa habari waandamizi nchini unaofanyika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga. "Ujangili bado ni tatizo kubwa, lakini tunashukuru mmeweza kulielezea mpaka watu wameweza kuogopa. Lakini bado tunataka muingie kwenye vita hii. Sio kwa kutumia bunduki, bali kalamu zenu. "Tunataka ile kauli ya Rais (Dkt. John Magufuli) itimie kuwa majangili wakiona tembo wawakimbie, lakini sio tembo kuwakimbia binadamu. Ni ukweli, kwa sasa mauaji kwa tembo wetu yamepungua, na majuzi tumeona mizoga ya tembo wawili Hifadhi ya Ruaha, na hiyo inatokana na wakati mwingine kufa kwa kuzeeka. "Tunajua, hata kwenye shirika letu la TANAPA bado kuna wafanyakazi wanawasaidia majangili kufanikisha malengo yao, lakini hao tutapambana nao, na siku tukiwabaini tutawatumbua" alisema Profesa Maghembe. Profesa Maghembe pia aliwataka waandishi wa habari kuwaeleza wananchi kuacha kuvamia hifadhi za misitu kwa minajili ya kupata maji na malisho, kwani kufanya hivyo kunaharibu mazingira, kusababisha migogoro, lakini pia kunaweza kusababisha magonjwa kati ya wanyamapori na wale wafugwao. "Wananchi waache shughuli zao kutoa nyumbani na kupeleka hifadhini. Bado tunaomba mtusaidie. Watu wasitake kuchanganya wanyama kwa kuona wote wana kwato. Hiyo sio kweli, wanyama wanakuwa na magonjwa mbalinbali kama ndigana, TB na kimeta" alisema Profesa Maghembe. Awali akimkaribisha mgeni rasmi kufungua, Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA Allan Kijazi alisema taasisi hiyo inayojitegemea imefanikiwa kwa kiasi kikubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 1959, kwani walianza na hifadhi moja ya Serengeti sasa zipo 16 hadi kufikia mwaka 2014. "Utalii unachangia asilimia 17.2 ya pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni nchini. Lakini pia, asilimia 80 ya utalii unatokana na hifadhi za Taifa. Pia TANAPA tunajitegemea kwa asilimia 100, na mchango wetu kwa Serikali umeongezeka kutoka sh. bilioni 27 mwaka 2015/16 mpaka sh. bilioni 34 kwa mwaka 2016/17 sawa na ongezeko la sh. bilioni saba" alisema Kijazi. Kijazi alisema Tanzania ina vivutio vingi vya kipekee ukilinganisha na nchi nyingine duniani. Shirika kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii nchini pamoja na ofisi za balozi zetu nchi mbalimbali itajitangaza ndani na nje ya nchi ili kuongeza idadi ya watalii.

Comments

Tanzania

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

Hatua za Ugonjwa wa UKIMWI

MAITI YAOKOTWA IKIWA KWENYE MFUKO, MIKONO NA MIGUU YAFUNGWA KAMBA KWA NYUMA