MAKAMU WA MWENYEKITI WA HALMASHAURI YA MBOWE WILAYA YA HAI ATIMKIA CCM


Makamu wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro ajiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) Katika hali isiyotarajiwa kwenye medani za siasa Mkoa wa Kilimanjaro na kipekee katika Wilaya ya Hai, leo tarehe 26 Julai 2017, Makamu wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai na Diwani wa Kata ya Machame Magharibi (Chadema) Ndugu Goodluck A. Kimaro ametangaza kuachana na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Pamoja na ndugu Kimaro, madiwani wengine wawili ndugu Evarist Kimathi Diwani wa Kata ya Mnadani na ndg. Abdalah Chiwili Diwani wa Kata ya Weruweru wameachia ngazi na uanachama kutoka Chadema. Katika Mkutano na waandishi wa habari ulioitwa na Ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Ndg. Iddi Juma, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimajaro Ndg. Jonathan Mabihya na viongozi wengine wa Chama kutoka Mkoa wa Kilimanjaro. Mgeni Rasmi katika shughuli hiyo ya kuwapokea viongozi hao wa Chadema alikuwa Ndg. H. H. Polepole Katibu wa NEC itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Akitoa neno la ukaribisho ndugu H.H. Polepole amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaheshimu uhuru wa maoni, uhuru wa mtu kushiriki siasa na kuwa na haki ya kujiunga na chama chochote cha siasa nchini. Akifafanua tukio la madiwani hao wa Chadema kuhamia CCM ameeleza "Viongozi hawa wameutumia uhuru na utashi wao wa kisiasa kufanya uamuzi sahihi, wamevutwa na kazi nzuri inayofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake katika kuwaletea wananchi watanzania maendeleo na wameamua kujiunga na jitihada za CCM na Serikali yake chini ya Uongozi wa Ndg. John Pombe Joseph Magufuli Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" Kwa upande wa viongozi hao ambao sasa ni wanachama wapya wa CCM wakitoa yao ya moyoni wamesema tarajio lao la kutimiza neno demokrasia katika chama hicho limepotea tangu awali kwa vitendo vya ubabe, umimi, ubinafsi, kupuuza matakwa ya wanachama na uongozi wa kiimla. Akisisitiza ndg. Kimathi amesema "hata wakati wa uchaguzi wa ndani wa Halmashauri ya Hai, aliyepasa kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ni Ndg. Kimaro na aliyepasa kuwa Makamu wa Mwenyekiti ni yeye (Kimathi) lakini kwa ubabe wa Mwenyekiti (Mbowe) walihujumiwa na kunyang’anywa nafasi zao" Ndugu H.H. Polepole ameikumbusha serikali ngazi ya Mkoa wa Kilimanjaro na vyombo vya Ulinzi na Usalama kuhakikisha ulinzi na usalama wa wananchi ikiwemo hawa unaendelea kuimarishwa, ikizingatiwa kumekuwapo na matukio ya kuwahujumu wananchi ambao wamehama Chadema na kujiunga na CCM. Viongozi hawa ambao wamejiunga na CCM leo ni mwendelezo wa viongozi wa vyama vya upinzani kuhama vyama vyao kwa msingi wa kuwa sehemu ya jitihada za kuwaletea maendeleo watanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali yake. Aidha ndugu H.H. Polepole ameendelea na vikao vya ndani vya ujenzi wa Chama na kuhamasisha Mageuzi Makubwa yanayofanywa na CCM na yenye lengo la kujiimarisha kama Chama cha wananchama na kinachoshughulika na shida za watu. Imetolewa na, IDARA YA ITIKADI NA UENEZI CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) Julai 26, 2017.

Comments

Tanzania

TAARIFA MBAYA KWA WAVUTAJI WA SIGARA, TUMBAKU

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

MADAI YA WAFANYAKAZI YASABABISHA VIFAA VYA UJENZI VYA KAMPUNI YA  CEYTUN KUZUIWA UWANJA WA NDEGE TABORA.