Msiwaonee haya viongozi wasiojali maendeleo, CCM waambiwa


Na Dismas Lyassa WANACHAMA wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kutowaonea haya viongozi ambao wanaonekana kutokuwa mstari wa mbele kushirikiana na wananchi katika kuharakisha maendeleo nchini. Kauli hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa Wanawake wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Mwanid Kiongoli akifungua rasmi mkutano uliokuwa na lengo la kuchagua viongozi wa wanawake katika Kata ya Pangani, wilayani Kibaha Mjini, Mkoa wa Pwani. “Rais wetu anataka maendeleo, mnamuona anavyofanya, anavyotembelea mikoa mbalimbali kusisitiza maendeleo, sisi tunatakiwa kumuunga mkono. Tumekuwa tukiona namna anavyowashughulikia wale ambao wanaonekana kutokwenda sawa na jitihada zake, hana mzaha, tunapaswa kwenda sambasamba na kasi hiyohiyo,” alisisitiza mwenyekiti huyo. Aidha aliwataka wananchi na wanachama kwa ujumla kutomuonea haya kiongozi au mtu yeyote ambaye kwa namna moja ama nyingine amepewa dhamana ndani au nje ya chama kuongoza chama au Serikali lakini hafanyi jitihada katika kuharakisha maendeleo. “Mtakuwa mnakosea sana kumuacha mtu ambaye mnamuona kabisa kwamba haendani na kasi yetu katika kuharakisha maendeleo kwenye ndani ya chama au nje ya chama,” alisema na kuongeza kwamba kama yuko ambaye anaonekana haendi sawa anapaswa kuombwa aachie ngazi. Alisisitiza kwamba ni kosa kubwa kumuonea haya mtu ambaye hasaidii kuharakisha maendeleo, kwani kumuonea haya ni kukiumiza chama na kuwaumiza wananchi ambao wanakiamini chama na kukipa nafasi ya kuendelea kuwa chama tawala. Nae Mwenyekiti wa CCM kata, Salum Msofe aliwataka wanachama kuendelea kuimarisha umoja wao kama mojawapo ya njia muhimu katika kudumisha maendeleo kwenye eneo lao, akisisitiza kwamba msingi wa kuwa na maendeleo ni kushirikiana. “Leo tunafanya uchaguzi kwa ajili ya kupata viongozi wa UWT kata, ni kazi ya wanachama kuchagua wale ambao inaamini watawasaidia katika chama na nje ya chama katika kuharakisha maendeleo kwenye eneo letu,” alisema na kuongeza kwamba wanawake wamekuwa watu muhimu katika maendeleo, hivyo wanatakiwa kufanya wanaliona linafaa katika uchaguzi. Kwa upande wake Katibu wa CCM Kata ya Pangani, Rashid Liunde aliwaomba wanachama kutokubali kushawishiwa kwa namna yoyote kuchagua watu kwa misingi yoyote isiyo na tija kwa maendeleo ya chama au eneo leo kwa ujumla. “Chagueni watu mnaoona wanafaa na wanaweza kusaidia chama na nchi katika kuleta maendeleo, yeyote anayewashawishi kwa njia mbaya, mnapaswa kutokubaliana nao,” aliwasisitiza Liunde. ********************

Comments

Tanzania

TAARIFA MBAYA KWA WAVUTAJI WA SIGARA, TUMBAKU

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

MADAI YA WAFANYAKAZI YASABABISHA VIFAA VYA UJENZI VYA KAMPUNI YA  CEYTUN KUZUIWA UWANJA WA NDEGE TABORA.