SERIKALI HAIJAFUTA MAFUNZO KWA WATUMISHI WA UMMA


SERIKALI HAIJAFUTA MAFUNZO KWA WATUMISHI WA UMMA Serikali haijafuta mafunzo kwa watumishi wa umma ambapo Taasisi za Serikali zimeelekezwa kuandaa Mpango wa Mafunzo kwa watumishi kwa njia ya uwazi na shirikishi ili kuepuka malalamiko kutoka kwa baadhi ya watumishi wa umma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) amesema hayo leo katika kikao kazi na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam. Mhe. Kairuki amesema mwajiri anapoandaa Mpango wa Mafunzo kwa watumishi wake ni vyema mpango huo ukawa shirikisha kwa watumishi wote ili kujua mpangilio wake, ikiwa ni pamoja na kuandaa orodha ya ziada ya watumishi watakaochukua nafasi za wale waliopangwa kushiriki mafunzo lakini wakashindwa. “Napokea malalamiko mengi sana kuhusiana na upendeleo katika suala la mafunzo, napenda kuwasisitiza waajiri tuandae Mpango wa Mafunzo ambao ni shirikishi kwa watumishi wote kuepuka haya, wengine wanapangwa na hawashiriki mafunzo,” Mhe. Kairuki amesema na kuongeza baadhi ya watumishi wa umma wanapangwa kushiriki mafunzo na hawaendi kwa sababu mbalimbali, lakini fursa ya nafasi hizo hawapangiwi wengine ili kuendana na mpango. Mhe. Kairuki ameongeza kuwa Mpango wa Mafunzo shirikishi pamoja na kuondoa malalamiko, utasaidia pia kutorudisha fedha zilizobaki kwa watumishi wa umma ambao walipangwa lakini wakashindwa kuhudhuria mafunzo kwa sababu mbalimbali. Aidha, Mhe. Kairuki amesema kwa sababu ya kutoshirikishwa wapo wanaopotosha kuwa Serikali imefuta Mpango wa Mafunzo. “Napenda kuwaambia kuwa Serikali haijafuta mafunzo, ili mtumishi wa umma aweze kufanya kazi zake kwa weledi ni lazima ahudhurie mafunzo,” Mhe. Kairuki amesema na kusisitiza Serikali inajali mafunzo kwa rasilimaliwatu kwa matokeo bora. Mhe. Kairuki yupo katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Dar es salaama ambapo leo ni siku ya nane akiwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa kukutana na watumishi wa umma wa kada zote katika vikao kazi. Lengo la kukutana na watumishi wa umma ni kusikiliza malalamiko, ushauri na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kuzifanyia kazi na kuleta mabadiliko katika Utumishi wa Umma nchini ili kufikia malengo yaliyopangwa na Serikali. IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI OFISI YA RAIS-UTUMISHI 19.07.2017

Comments

Tanzania

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

Hatua za Ugonjwa wa UKIMWI

MAITI YAOKOTWA IKIWA KWENYE MFUKO, MIKONO NA MIGUU YAFUNGWA KAMBA KWA NYUMA