Mahakama ya Afrika yaanzisha mpango wa msaada wa kisheria kwa watu wasiokuwa na uwezo


Arusha, 2 Augusti 2017 (EANA)--Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na watu(AfCHPR) imeanzisha mpango wa msaada wa kisheria kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kulipia huduma za kisheria wanaopeleka mashauri yao katika Mahakama hayo. Ili kufanikisha mpango huo,AfCHPR imeanzisha mafunzo kwa wanasheria 40 waliojiandikisha katika Mahakama hiyo ya Afrika ya Haki za Binadamu na watu kwa lengo la kuwawakilisha baadhi ya watu katika kesi zao Mahakamani hapo lakini hawana uwezo wa kulipia huduma za kisheria. Kwa mujibu wa Rais ya Mahakama hiyo Jaji Sylvain Ore’,mafunzo hayo yatakayofanyika kuanzia August 3 (Kesho, Alhamisi) hadi 5,Mwaka huu jijini Arusha yaliko Makao makuu ya Mahakama hiyo, yanalenga kuwapa fursa wanasheria hao kufahamu kwa undani uendeshaji wa shughuli za kisheria Mahakamani hapo na pia mchakato wa mpango wa msaada wa huduma za kisheria. “Hii ni mara ya kwanza kwa AfCHPR kuendesha mafunzo ya aina hiyo” alisema Jaji Ore’ na kuongeza kuwa mwishoni mwa mafunzo hayo wanasheria husika watapanua maarifa yao yatakayosaidia kuwawakilisha vema mahakamani hapo watu wasiokuwa na uwezo. Katika kuhakikisha kuwa mpango huo wa huduma za kisheria kwa wapeleka mashauri wasio na uwezo wa kulipia aliyekuwa Rais Mstaafu wa awamu ya 4 wa Tanzania,Dk.Jakaya Kikwete alichangia dola za kimarekani 100,000 wakati wa ziara yake Mahakamani hapo Novemba,2015. Hadi sasa,Jumla ya Mawakili 61 kutoka nchi 25 wamejiandikisha katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na watu kwa lengo la kuwawakilisha watu wasiokuwa na uwezo kulipia huduma za kisheria. Mawakili hao 61 wanatoka nchini Algeria,Benin,Mali,Burundi,Cameroon,Congo(DRC),Misri,Uholanzi na Ufaransa.Nchi zingine ni  Gabon,Gambia,Italia,Kenya,Liberia,Mali,Mauritania,Nigeria,Rwanda,Senegal,Afrika Kusini,Tanzania,Togo,Uganda,Uingereza,Marekani,Zambia na Zimbabwe. Hadi katikati ya mwezi Julai,2017 AfCHPR ilikuwa imepokea mashauri 147 ambapo kati ya hayo,mashauri 134 yalitoka kwa watu binafsi,10 yalitoka Mashirika yasiyo ya kiserikali(NGO’s) na 3 yalitoka kamisheni ya Banjul. Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ilianzishwa kwa mujibu wa Kifungu Namba Moja cha itifaki ya Mkataba wa Mahakama hiyo kwa lengo la kuimarisha jukumu la kulinda haki za Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu barani Afrika. Na Kulwa Mayombi, EANA

Comments

Tanzania

TAARIFA MBAYA KWA WAVUTAJI WA SIGARA, TUMBAKU

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

MADAI YA WAFANYAKAZI YASABABISHA VIFAA VYA UJENZI VYA KAMPUNI YA  CEYTUN KUZUIWA UWANJA WA NDEGE TABORA.