Mazoezi ya pamoja ya SADC yataongeza ushirikiano


Na Mashaka Mhando,MUheza WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt Hussein Mwinyi, amesema mazoezi ya pamoja kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), yatasaidia kujenga ushirikiano baina ya nchi hizo ikiwemo kupeana ujuzi na udhoefu wa vyombo hivyo vya ulinzi. Akifungua mazoezi hayo yanayojulikana 'Excise Matumbawe', katika kijiji cha Mlingano kilichopo kata ya Mlingano, Waziri Dkt Mwinyi alisema mazoezi hayo yatawajenga wanajeshi utimamu ikiwa ni pamoja na kuongeza udhoefu miongoni mwao lakini pia watapata mazoezi ya kukabiliana na majanga mbalimbali. "Kwanza tunashukuru kwa uongozi wa SADC kututeua mwaka huu tuwe wenyeji wa mazoezi haya ya pamoja ambayo tunaamini yataleta ushirikiano zaidi katika nchi zetu lakini pia wapiganaji watapata udhoefu na kubadilishana ujuzi," alisema Dkt Mwinyi. Alisema ni muhimu kwa wanajeshi kujiweka katika utayari wa kukabiliana na matukio mbalimbali kama ambavyo lengo la mazoezi hayo ni kujifunza mbinu za kukabiliana na masuala ya ugaidi, uharamia na majanga yatakayozikumba nchi hizo wanachama. Dkt Mwinyi alisema kuwa mazoezi hayo yatasaidia nchi hizo kusaidiana katika kulinda amani ikiwemo kusaidiana katika kuhakikisha zinatekeleza mipango mbalimbali ya kuzuia na kupambana na vitendo vinavyoweza kuleta machafuko katika nchi hizo. Akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri huyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Generali Venanche Mabeyo, alisema kwamba katika kipindi ambacho wanajeshi hao watakuwa katika mazoezi hayo, wananchi watanufaika na huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo kutoa huduma za afya, kusaidia kurekebisha miundombinu ya chuo cha kilimo Mlingano. Alisema SADC kama kanda maalum katika nchini hizo zinachukua mazoezi ya kukabiliana na vitisho vyovyote katika nchi mwanachama na endapo nchi moja itakabiliwa na matatizo hayo zitasaidiana kwa pamoja katika kutekeleza au kupambana na adui. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela alisema kuwa mazoezi hayo hayana uhusiano na matukio yoyote yale nchini na amewaomba wananchi watoe ushirikiano kwa wanajeshi na wasiokote kitu chochote kinachoonesha kuwa ni cha kijeshi. Nchi zinazoshiriki mazoezi hayo ambayo mara ya mwisho yalifanyika nchini Zimbabwe 'Excise Mahombekombe', ni kutoka Botswana, Lesotho, Malawi, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe na wenyeji Tanzania. Nchi nyingine zinazounda umoja huo hazikuweza kuja kutokana na mambo mbalimbali. MWISHO

Comments

Tanzania

TAARIFA MBAYA KWA WAVUTAJI WA SIGARA, TUMBAKU

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

MADAI YA WAFANYAKAZI YASABABISHA VIFAA VYA UJENZI VYA KAMPUNI YA  CEYTUN KUZUIWA UWANJA WA NDEGE TABORA.