PROGRAMU YA UMEME VIJIJI YAANZA KULETA MATUMAINI YA MAGEUZI KATIKA SEKTA  MBALIMBALI MKOANI TABORA 


Na Tiganya Vincent.   SERIKALI  ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano tangu iingie madarakani Desemba 2015 ililenga kuhakikisha kuwa wananchi wote wa Tanzania wananufaika matunda ya nchi yao katika Nyanja mbalimbali ikiwemo hupatikanaji na huduma za maji , umeme , elimu , afya  na uchumi kwa usawa.   Hali hii inajidhihirisha wakati Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani baada ya kuzindua Awamu ya Tatu ya Usambazaji wa Umeme Vijiji (REA III) mkoani Tabora ambapo vijiji 510 vitaunganishwa na huduma hiyo ifikapo mwaka 2021.   Akizungumza wakati wa uzinduzi wa awamu hiyo anasema kuwa Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) inatarajia kuunganisha jumla ya vijiji 7873 nchini kote na vitongoji vyake vyote  hapa nchini vitakuwa vimeshaunganisha na umeme chini ya Mradi wa Umeme Vijijini Awamu wa Tatu ifikapo mwaka 2021. Dkt. Kalemani anasema REA III itasaidia  kuunganisha umeme katika vijiji vilivyobaki ambavyo havijaunganishwa na umeme ifikapo mwaka 2021 kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya uchumi kati kuelekea uchumi wa viwanda. Anasema kuwa lengo la Serikali ni kutaka wananchi wote hata wale wanaoishi visiwani waweze kufikiwa na huduma ya umeme kwa ajili ya matumizi yao na kwa ajili ya uendeshaji wa viwanda. Aidha kwa upande wa Mkoa wa Tabora anasema vijiji vipatavyo 510 na vitongoji vyake vinatarajiwa kuwa vimeshaunganishwa na umeme wa uhakika wa ifikapo mwaka 2021 kupitia mradi wa REA III. Dkt. Kalemani anasema kuwa sehemu ya awali ya utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya Umeme Vijijini katika Mkoa wa Tabora utahusisha upelekaji wa umeme katika vijiji 173 kwa gharama ya shilingi bilioni 60.39.   Anasisitiza kuwa utekelezaji wa sehemu hiyo ya kwanza ambao umeanza mwanzoni mwa mwaka huu 2017 unatarajia kukamilika ifikapo mwezi Aprili mwaka 2019. Naibu Waziri huyo anasisitiza kuwa katika kuhakikisha kuwa mradi huo wa upelekaji umeme katika vijiji vya Mkoa wa Tabora unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa Serikali imeingia mkataba na kampuni za Pomy Engineering Company  Limited , Intercity Builders Limited na Octopus Engineering Limited ambazo zitatekeleza mradi huo kwa umoja. Anaongeza kuwa ili kuhakikisha lengo hilo la kuunganisha vijiji vyote vinakuwa na umeme, Wakandarasi  hao watashirikiana na Wakandarasi wazawa wa eneo husika ambao wanasifa ili kurahisisha kazi na kuifanya iwe na ufanisi. Aidha Dkt. Kalemani anaongeza kuwa sehemu ya pili ya mradi huu wa kusambaza umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa vijiji vilivyobaki 337 vya Mkoa wa Tabora utaanza kutekelezwa baada ya kukamilika kwa sehemu ya kwanza mwaka 2019 na kukamilika ifikapo 2021. Anatoa wito kwa wananchi kuanza kujiandaa kutumia fursa ya umeme vijiji katika kujenga viwanda mbalimbali kama vile vya kusindika mazao , kuanzisha mashine za kusaga nafaka, kufidhi chakula na viwanda vya useremali kwa ajili ya kujiingizia kipato na kuboresha maisha yao. Naibu wa Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Kalemani anasema sanjari na hilo ni vema Serikali kuanzia vijiji hadi Mkoa kuanza kubainisha maeneo maalum ya viwanda ya vidogo na vikubwa ambayo  mradi wa REA III utafikisha miundo mbinu ya umeme kwa ajili ya uendeshaji wa Viwanda. Aidha , Dkt. Kalemani anasisitiza kuwa Serikali imetumia gharama kubwa katika kuhakikisha kuwa wananchi waishio vijijini nao wananufaika na huduma ya umeme kama walivyo wa mijini kwa kuanza kujenga miundo mbinu na kuwaunganishia umeme kwa hiyo zoezi hilo halina fidia hasa wale ambao maeneo yao nguzo zitapita. Anatoa wito kwa wananchi wasichelewesha mradi kwa kudai fidia ambayo haipo na kufanya hivyo ni kuwacheleweshea wananchi wenzao maendeleo.   Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri anasema kukamilika kwa mradi wa REA III utaufanya mkoa huo kukua kwa kasi zaidi na kutoa wito kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika viwanda vya sekta mbalimbali ikiwemo za usindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo na uchimbaji madini. Anasema kuwa hivi sasa Mkoa huo unazidi kuimarika katika miundombinu ya barabara , reli , anga na upatikanaji wa maji  na umeme wa uhakika na hivyo kutokuwepo na vikwazo katika uzalishaji. Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Mwanri amewapongeza Viongozi wa Kitaifa kwa upendo wao kwa Mkoa wa huo kwa kupeleka miradi mbalimbali ikiwemo ule wa maji toka ziwa Victoria wenye gharama ya bilioni 601 , ujenzi wa barabara, upanuzi wa uwanja wa ndege na hatimaye usambazaji wa umeme vijijini awamu ya tatu.   Anawaomba wananchi wa Mkoa wa Tabora kuacha kuchoma moto ovyo na kusababisha kuunguza mistu ikiwemo nguzo za umeme na kulisababishia hasara Shirika la TANESCO na Taifa kwa ujumla.   Mkuu wa huyo wa Mkoa anawaonya kuwa wananchi watakaodai fidia kwa nia ya kukwamisha mradi kuacha mara moja hatua hiyo kwani uongozi wake hautakubali hilo.   Anasema hawezi kukubali kuhamishwa kwa mradi kwa sababu ya watu wachache kudai fidia kwa kuwa nguzo za umeme zimepita katika mashamba yao na kuongeza kuwa hatakubali hilo litokee kwa kuwa linakwamisha maendeleo na adhima ya Serikali ya ujenzi wa Viwanda.   Bw.Mwanri anaongeza kuwa mara popote ambapo umeme umeingia kunakuwepo na nuru ya maendeleo na hivyo ni vema wananchi wakatoa ushirikiano kwa kampuni zote zizokabidhiwa jukumu la ujenzi wa miundo mbinu ili kazi hiyo isichelewe na kuzorotesha maendeleo ya wananchi wengi ambao wanataka kuchangamkia fursa hiyo.     Naye Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (REA) Mhandisi Gissima Nyamo-hanga anasema kuwa awamu ya tatu ya usambazaji wa umeme vijijini unalenga kufikisha huduma ya umeme kwenye vijiji 7,873 katika mikoa na wilaya zote za Tanzania Bara ambazo hazijafikiwa umeme.   Anasema kuwa taarifa ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaaa(TAMISEMI) inaonyesha kuwa Tanzania bara ina vijiji 12,268 ambapo ni 4,395  ndio vilivyofikiwa umeme hadi kufikia mwaka 2016 ambavyo ni sawa na asilimia 36 ya vyote ndivyo vinavyopata huduma hiyo muhimu.   Mhandisi Nyamo Hanga anasema kuwa kati yake vijiji  7,873 ndio havijapata umeme wakati 7,697 vimepangiwa kupata umeme wa gridi wakati 176 pamoja na visiwa vitapatiwa umeme wa nje (off grid) kwa kuwa ndio njia muafaka ya kuvipatia kwa sasa.   Anasisitiza kuwa mradi huo umepangwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka huu wa fedha na hatimaye kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2020/21.   Mhandisi Nyamo hanga anasema kuwa utekelezaji wa mradi huo utajumuisha vipengele vya kufikisha umeme kwenye vijiji ambavyo havijafikiwa kabisa miundombinu ya umeme wa gridi ya taifa, kuongeza wigo wa usambazaji wa umeme kwenye vijiji ambavyo vimefikiwa umeme lakini si wananchi wote wanapata huduma hiyo na usambazaji wa nishati jadidifu(renewable energy) kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi ambayo ni vigumu kufikiwa.   Mbunge wa Jimbo la Sikonge anawaomba wakazi wa jimbo lake kutoa ushirikiano kwa watu wote ambao mradi ukapopitia ili hatimaye ukamilike kwa wakati kwani unalenga kuwaondoa katika umaskini kwa kuwa na fursa za kufungua miradi mbalimbali za kujiingizia kipato.   Anasema kuwa ushirikiano wa wananchi na Kampuni zinajenga miundo mbinu ya umeme utasaidia Serikali kupeleka katika maeneo mengine na kusaidia Taifa hilo kuwa na maeneo mengi yanayopata huduma hiyo.   Naye Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Abel Busalama anasema kuwa umeme ni kitu muhimu katika maisha ya mwanadamu na kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Tanzania, hivyo uzinduzi wa Awamu ya Tatu ya Umeme vijiji katika kijiji cha Kisanga ni fursa ya kuleta mabadiliko chanja kwa wakazi wa Mkoa wa Tabora.   Anaipongeza Serikali kwa uzinduzi huo kwani utainufaisha Wilaya yake ambapo Vijiji 25 kikiwemo cha 2784 vitanufaika na raundi ya kwanza ya Awamu hii ya Tatu.   Mkuu wa Wilaya wa Sikonge Peres Magiri anasema kuwa kukamilika kwa mradi wa REA III katika wilaya hiyo kutasaidia usambazaji wa huduma ya maji katika maeneo mbalimbali na kuwapunguzi adha wananchi ya kufuata maji katika vyanzo wa maji.   Anasema kuwa awamu hiyo itasaidia vijiji 41 kupata huduma ya umeme na kubaki 30 ambapo hadi 2021 vitakuwa vimefikiwa.   Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Simon anasema kuwa kupelekwa kwa umeme katika vijiji vya mkoa wa Tabora ambavyo vilikuwa havina huduma hiyo utasaidia kuleta maendeleo kwa wakazi wake kuanzisha fursa mbali za kujiingizia kipato ikiwemo kuendesha huduma za vinywaji mbalimbali.   Anasema huduma hiyo itasaidia kufikia kuanzisha viwanda kama vile vya usindikazaji wa zao la tumbaku kwa kuwa eneo hilo ni wazalishaji wa zao hilo na vyama vyao vya msingi viko imara na kunaupatikanaji wa huduma na maji ya uhakika.   Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge anasisitiza kuwa umeme kwa kuwa umefika katika eneo hilo basi maendeleo nayo yamefika.   Naye Meneja Mwandamizi wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO)  wa Kanda ya Magharibi Markin Mbonile anasema kuwa watajitahidi kuhakikisha kuwa umeme unaenea katika maeneo mengi hapa nchi kwa ufadhili wa REA.   Anasema kuwa katika kuhakikisha kuwa zoezi hilo linafanikiwa TANESCO wamejipanga kuhakikisha kwamba katika kila ngazi ya utekelezaji wa mradi kutakuwa na mtu mmoja ambaye kila siku jukumu lake kuwa ni kusimamia mradi na mawazo yake kila wakati ni mradi.   Meneja huyo anawasa wakazi wa vijijini kutumia fursa ya upatikanaji wa umeme vijijini kujiandaa katika uanzishaji viwanda vidogo vidogo ili waweze kunufaika na huduma hiyo kwa ajili ya kujiletea maendeleo na uchumi wa taifa unaimarika.   Anasema kuwa ni Serikali kupitia TANESCO na kwa kuzingatia nishati ya umeme imepunguza gharama za kuunganishiwa umeme kwa mteja ambapo itakuwa shilingi milioni 27,000/- kwa wateja wa vijijini na fedha hizo zitalipwa katika Ofisi hizo.   Kwa upande wa Kiongozi wa Kampuni za Pomy Engineering Company  Limited , Intercity Builders Limited na Octopus Engineering Limited Mhandisi Eva Fumbuka  ambazo zitatekeleza mradi huo kwa umoja  anasema kuwa watahikikisha wanamaliza mradi kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa. Anasema kuwa zoezi hilo limeanza wiki  hii ambapo wataanza kufanya uchunguzi (survey) katika wilaya zote za Mkoa wa Tabora na baada ya zoezi hilo matokeo yake watayapeleka katika Ofisi za REA kwa ajili ya uidhinishaji ili waendelee na taratibu nyingine za manunuzi. Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kata ya Kisanga Wilayani Sikonge Juma Katangwa anaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutekeleza ahadi ya kupeleka umeme katika eneo lao ambapo wakazi wa eneo hilo watanufaika na fursa mbalimbali zinazotokana na uwepo wa umeme katika eneo lao kama vile kuanzisha saloon , uuzaji wa juice na ujenzi wa mashine za umeme za kusaga.   Anasema uwepo wa umeme katika eneo lao utasaidia kupunguza gharama za maisha ambapo wakazi wa eneo hilo walikuwa wakilazimika kutumia zaidi ya shilingi 15,000/ kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya taa kwa mwezi.   Kwa upande wa Mariam Juma anasema kuwa kitendo cha Serikali kuzindua awamu ya Tatu ya REA katika eneo lao la kuwahakikisha kuwa wataunganishiwa umeme kimempa imani kubwa na Serikali ya Awamu ya Tano na hivi sasa anataraji kuanzia saloon ya wanawake na duka la vinywaji.   Anasema kuwa hatua hiyo inalenga kuwapunguzi adha za wakinadada kusafiri umbali wa kilometa zaidi ya 10 kutoka Kisanga hadi Sikonge kutafuta huduma za kutengenezwa nywele pindi anapokuwa na shughuli kama vile harusi.   Uzinduzi wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mkoani Tabora umefanyika katika Kijiji cha Kisanga , wilayani Sikonge kwa niaba ya Vijiji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa.   MWISHO

Comments

Tanzania

TAARIFA MBAYA KWA WAVUTAJI WA SIGARA, TUMBAKU

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

MADAI YA WAFANYAKAZI YASABABISHA VIFAA VYA UJENZI VYA KAMPUNI YA  CEYTUN KUZUIWA UWANJA WA NDEGE TABORA.