Rais Shein aipongeza Bodi Benki ya Watu wa Zanzibar


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, ametoa pongezi kwa Bodi ya Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na uongozi wa Benki hiyo kwa mafanikio iliyoyapata na kuitaka kujiendesha kibiashara ili ipate kuimarika zaidi. Dk. Shein aliyasema hayo, alipokutana na Uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), pamoja na uongozi wa Bodi ya PBZ katika vikao vinavyoendelea Ikulu mjini Zanzibar. Katika vikao vya leo, Dk. Shein kwa nyakati tofauti alikutana na Uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bodi ya Wakurugenzi ya PBZ na uongozi wake pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Bima na uongozi wake. Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa licha ya changamoto zilizojitokeza lakini Benki hiyo imeweza kupata mafanikio makubwa na kusisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja hatua ambayo itasaidia kuiendeleza Benki hiyo. Akitoa maelezo yake Dk.Shein alisema kuwa wafanyakazi Benki hiyo ni lazima wafuate maadili, sheria na taratibu za kazi na kuutaka uongozi kuwapongeza kwa wale wanaofanya vizuri. Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Dk. Khalid Mohamed alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa miongozo anayoitoa kwa Wizara hiyo na kupongeza hatua zilizofikiwa na PBZ kwa kumiliki asilimia 41 ya mikopo kwa Soko la Mabenki hapa Zanzibar kwa mwaka 2016 hatua inayoonesha jinsi Benki hiyo inavyoaminiwa. Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee kwa upande wake alitoa pongezi kwa hatua kubwa iliyofikiwa na Benki hiyo sambamba na kusisitiza haja kwa Benki hiyo kuwa Serikali ina matumaini makubwa na chombo hicho kwani ni chanzo kimojawapo cha kuiongezea mapato yake. Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan alieleza kufarajika kwake na maendeleo makubwa yaliopatikana na PBZ na kueleza haja ya kuifuata na kuitekeleza Sheria iliyounda Benki hiyo pamoja na zile zinazoenda sambamba na sheria hiyo. Mapema Mwenyekiti wa PBZ Abdulrahman Mwinyimbegu alieleza kuwa kuongezeka kwa matawi kumesaidia kupata wateja wengi na hivyo amana za wateja zimeongezeka kutoka TZS 33 bilioni mwaka 2001 hadi kufikia TSZ 427 bilioni mwaka 2016. Alieleza kuwa hadi kufikia mwezi Juni 2017 Mtaji halisi umefikia TZS 50 bilioni na PBZ inatarajia hadi mwishoni mwa mwaka huu mtaji halisi utafikia TZS 58 bilioni. Aliongeza kuwa Bodi ya Wakurugenzi kwa kushirikiana na Uongozi wa PBZ katika mpango wake wa baadae imepanga kutekeleza baadhi ya miradi katika kipindi kitakachomalizikia mwaka 2020 ikiwemo kuweka mtandao mpya wa kibenki, kuimarisha huduma za kimtandao. Miradi mengine ni kuanzisha mfumo wa kukusanya mapato ya Serikali kwa njia ya kielektroniki, uanzishwaji wa biashara ya kadi za Mastercard, kuongeza idadi ya matawi kwa kufungua matawi huko Dodoma na Dar es Salaam pamoja na kujenga jengo la Makao Makuu Mazizini. Mkurugenzi Mtendaji wa (PBZ) Juma Ameir alieleza kuwa mapato ghafi ya benki yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka TZS 16 bilioni katika mwaka 2011 hadi kufikia TZS 58 bilioni mwaka 2016 ambapo kiwango hiki ni zaidi ya makadirio ya TZS 55 bilioni kwa mwaka 2016. Aliongeza kuwa amana za wateja zimeongezeka kutoka TZS 140 bilioni mwaka 2011 hadi kufikia TZS 427 bilioni mwaka 2016 ambapo hata hivyo Benki inatarajia kuwa na amana za wateja zenye kufikia thamani ya TSZ 478 bilioni ifikapo Disemba mwaka 2017 . Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Bima na Uongozi wake na kumpongeza Waziri kwa kulisimamia vyema Shirika hilo pamoja na mashirikiano makubwa yaliopo katika Bodi na uongozi wa Shirika hilo ulipelekea kupata mafanikio makubwa. Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwepo Idara itakayoshughulikia suala zima la mafunzo kwa wafanyakazi za Shirika hilo. Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alieleza haja ya kutoa elimu kwa jamii ili wapate uwelewa juu ya umuhimu mkubwa wa kuwa na Bima katika mali zao kutokana na umuhimu wake. Nae Mwenyekiti wa Shirika la Bima Jumbe Said Ibrahim alieleza kuwa mapato kwa kipindi cha miaka mitatu 2014 hadi 2016 yameongezeka kutoka TZS bilioni 17 hadi bilioni 19 mwaka 2016 ambapo alieleza kuwa licha ya kuongezeka kwa mapato Shirika hilo limelipa TZS bilioni 6 kwa madai ya maumivu, vifo, uharibifu wa mali, moto na mengineyo. Mwenyekiti huyo alieleza kuwa mbali ya huduma za Bima, Shirika hilo limekuwa likitoa huduma zake kwa ukaribu na jamii pamoja na kutoa misaada mbali mbali katika sekta ya afya, elimu na wananchi kwa jumla. Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima Abdulnasir Ahmed Mohammed alieleza kuwa mtaji wa Bima kwa mashirika ya Bima unaongezeka kila mwaka kwa mujibu wa Sheria namba 10 ya mwaka 2009. Akitoa ushauri wa Shirika hilo kwa taasisi nyengine Mkurugenzi huyo alisema kuwa kuna haja ya kuangalia upya utoaji wa leseni za madereva hususan vijana, kuwa na sheria kali kwa wale wanaoendesha vyombo kwa kasi na kwa wale wanaopakia mizigo na abiria wengi kupindukia, kuwepo vifaa vya kuzimia moto maofisini. Ushauri mwengine ni vyombo vya baharini visiruhusiwe kubeba abiria mpaka vipate vibali maalum na viwe vinafanyiwa uchunguzi kila mara, umri wa madereva wanaoendesha magari ya abiria usipungue miaka 30 na kuendelea, iwapo ajali itatokea dereva mwenye gari asiruhusiwe kuchukua gari yake mpaka jeshi la Polisi litakapofika kwa ukaguzi wa gari pamoja na madereva wanaosababisha ajali mara kwa mara kunyanganywa leseni ya udereva na kupewa adhabu. Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

Comments

Tanzania

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

Hatua za Ugonjwa wa UKIMWI

MAITI YAOKOTWA IKIWA KWENYE MFUKO, MIKONO NA MIGUU YAFUNGWA KAMBA KWA NYUMA