SSRA YAFUNGUA MILANGO KWA WAKULIMA


Na Nazael Mkiramweni, Dodoma.   MAMLAKA ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) imefungua milango kwa wakulima kujiunga na mifuko ya Hifadhi za jamii nchini ili waweze kujiwekea akiba ya uzeeni.   Uamuzi huyo wa SSRA utawawezesha wakulima kujiwekea akiba ambazo watazitumia watakapokosa uwezo wa kulima na kujihifadhi mazao kwa ajili ya matumizi ya chakula pamoja na biashara.   Akizungumza jana na mwandishi wa habari hii katika viwanja vya Nanenane, Meneja Mawasiliano wa SSRA, Sarah Msika alisema wameshiriki katika  maonyesho hayo ya wakulima kwa kusudi kubwa la kuhamasisha wakulima kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo kwa sasa ipo kwa ajili ya watu wote.   Alisema kwa mujibu wa  sheria ya SSRA  sura ya 135 kifungu kidogo cha  tano, kazi ya Mamlaka hiyo ni kulinda na kutetea maslahi ya wanachama hivyo walilazimika kubadilisha mfumo wa Mifuko ya hifadhi za jamii ili iweze kuwajumuisha watu ambao wamejiajiri wenyewe.   “Mifuko ya Hifadhi za Jamii kwa sasa ipo kwa ajili ya wafanyakazi walio katika sekta rasmi na isiyo rasmi wakiwemo wajasiriamali, wakulima, wavuvi, wakulima, waendesha bodaboda na wote wenye kipato,”alisema Msika.   Alisema sera ya hifadhi ya jamii ya mwaka 2003 inaeleza wazi kuwa hifadhi ya jamii ni kwa kila mtu mwenye kipato wakati Katiba ya mwaka 1977 inaeleza kuwa kujiunga kwenye mifuko hiyo ni haki ya kila mtu.   “Tanzania ina watu milioni 25 wenye shughuli za kuwapatia kipato wakiwemo wakulima lakini waliojiunga na mifuko ya hifadhi ya Jamii ni takribani milioni 2.4” alisema.   Katika  hatua nyingine SSRA imeunga mkono hatua ya serikali kuhamishia makao yake makuu mkoa hapa kwa kufungua ofisi mkoani hapa kwa lengo la kuhakikisha wanachama wa kanda ya kati wanapatiwa huduma kiurahisi.   “Ofisi hiyo pia itarahisisha wanachama na wastaafu kutatuliwa kero zinazowakabili katika huduma wanazozipata kutoka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii”alisema Msika.   Mwisho.

Comments

Tanzania

TAARIFA MBAYA KWA WAVUTAJI WA SIGARA, TUMBAKU

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

MADAI YA WAFANYAKAZI YASABABISHA VIFAA VYA UJENZI VYA KAMPUNI YA  CEYTUN KUZUIWA UWANJA WA NDEGE TABORA.