DOKTA MPANGO AIHIMIZA WAINGEREZA KUKUZA ZAIDI BIASHARA NA UWEKEZAJI NCHINI


Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam Tanzania imetoa rai kwa Serikali ya Uingereza kubadili mfumo wa uhusiano wake kwa kujikita zaidi katika masuala ya biashara na uwekezaji badala ya kutoa misaada ya kawaida ili nchi iweze kukuza uchumi wake kwa haraka zaidi. Wito huo umetolewa Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa wabunge kutoka mabunge ya uingereza (Baraza la Mamwinyi na Bunge la Wawakilishi). Dokta Mpango amesema kuwa kiwango cha mtaji ambacho Serikali ya Uingereza imewekeza nchini hadi sasa ni Paundi bilioni 2.5 lakini kwa upande wa biashara kati ya nchi hizo mbili, hali si nzuri. "Mwaka 2015 Tanzania iliuza nje bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 22.5 na kununua bidhaa kutoka Uingereza zenye thamani ya Dola milioni 150, kiwango ambacho ni kidogo sana na tunahitaji kufanya biashara zaidi" Alisisitiza Dkt. Mpango. Alielezea hatua mbalimbali ambazo Serikali inazichukua kuimarisha uchumi wa viwanda na kuelezea changamoto kubwa ikiwa na namna ya kuendeleza kilimo kwa ajili ya kupata malighafi za viwanda na kuwainua wananchi kiuchumi kwa kuwa kilimo ndicho kinaajiri idadi kubwa ya Watanzania. Dkt. Mpango alitoa wito kwa Serikali ya Uingereza kuwekeza zaidi katika viwanda vitakavyoongeza thamani ya bidhaa mbalimbali ikiwemo kujenga viwanda vya kutengeneza matrekta na zana nyingine za kilimo, kusindika bidhaa za mazao ya wakulima pamoja na kuwekeza katika sekta za kuongeza thamani ya madini na nishati ya umeme. Dokta Mpango aliwaeleza Wabunge hao kwamba hivi sasa Serikali imepiga hatua kubwa kiuchumi na kuishukuru Uingereza kwa mchango mkubwa inaoutoa kusaidia Elimu, Lishe, Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma na afya kwa upande wa lishe, uwekezaji ambao kwa pamoja umefikia zaidi ya paundi milioni 180. Kwa upande wake, kiongozi wa Wabunge watano waliomtembelea Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa David Linden, amesema wamefurahishwa na namna Tanzania inavyopiga hatua kubwa kimaendeleo na kudhibiti vitendo vya rushwa. Amesema kuwa wameridhishwa na kiwango cha miradi wanayoifadhili katika sekta ya elimu na afya hususan masuala ya lishe kwa watoto na kwamba nchi yao itaendelea kuisaidia Tanzania ili iweze kufikia malengo yake kiuchumi na kijamii Wabunge hao wapo nchini tangu Jumapili iliyopita na wanatembelea miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Serikali ya Uingereza. Mwisho

Comments

Tanzania

TAARIFA MBAYA KWA WAVUTAJI WA SIGARA, TUMBAKU

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

MADAI YA WAFANYAKAZI YASABABISHA VIFAA VYA UJENZI VYA KAMPUNI YA  CEYTUN KUZUIWA UWANJA WA NDEGE TABORA.