JPM: NYERERE ALISEMA SAFARI YA KUJENGA NCHI YA HAKI NA KUONDOA DHULUMA NI NGUMU


JPM: NYERERE ALISEMA SAFARI YA KUJENGA NCHI YA HAKI NA KUONDOA DHULUMA NI NGUMU •Usisikilize kelele za wanaokuzoza wapeleke Watanzania kwenye nchi ya Asali na Maziwa. •Safari hii itakujengea maadui kwa kuwa wanaoichukia haki na wapenda dhuluma ni wengi Na Mwandishi Wetu- MAELEZO Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amepokea ripoti ya uchunguzi madini ya Almasi na Tanzanite chini ya Kamati zilizoundwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwasilishwa Ikulu na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa. Akikabidhi taarifa hizo, Waziri Mkuu amesema; “Bunge linatoa ushauri mzuri kwa serikali kuhusiana na kulinda rasilimali zetu, hasa madini na leo tunabidhi ripoti ya Uchunguzi wa Almasi na Tanzanite kwa Mhe Rais ambaye ametaka ripoti hizo za madini ziwekwe wazi ili wananchi wajue mwenendo mzima wa rasilimali zao. Makala yangu inaangazia hotuba ya Hayati Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyoitoa katika kilele cha sherehe za Sikukuu ya Wafanyakazi, maarufu Mei mosi Mkoani Tabora mwaka 1981. Katika mkutano huo, hotuba yake iliambatana na hadithi fupi na tamu yenye maana kubwa na funzo kwa viongozi wetu na Watanzania kwa ujumla. Ambapo, Mwenyekiti wa Kamati ya kuchunguza Almasi Mhe. Dotto Biteko aliinukuu wakati wa kukabidhi taarifa hiyo kwa Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai. Mwalimu anasimulia; Kulikuwa na Binti mzuri kabisa aishiye mlimani na wazazi wake, ambaye alikuwa anataka kuposwa na vijana mbalimbali, lakini vijana hao bila mafanikio walishindwa kufika mlimani anapoishi binti huyo, kutokana na kushindwa kutimiza masharti waliyopewa na Bibi kizee ambaye alikuwa anaishi chini ya mlima ule. Bi kizee huyo alitoa masharti ya kufika pale mlimani lakini vijana wengi walishindwa kutii maelekezo na masharti ya kutogeuka nyuma wanaposikia makelele ya kuzomea na kuzoza. Kabla ya safari Bibi anawaaasa vijana hao kuwa imara na kutosikiliza makelele hayo, bali moja kwa moja waende bila kugeuka nyuma mpaka wafike mlimani na kutimiza azma yao ya kumpata binti huyo. Mwalimu akisimulia masharti ya Bi kizee amesema: Bi kizee alimuuliza kijana yule wa mwisho aliyekuwa mdogo na mnyonge unakwenda wapi, kijana alijibu naomba unielekeze kule nitakakompata binti yule akaaye kilimani ili niweze kumuoa. Bibi kizee aljibu kijana nadhani ni busara ukarudi kwa kuwa sio rahisi kufika pale kilimani, vijana wenzako waliotangulia wameshindwa kufuata masharti niliyowapa na kugeuka jiwe la chumvi. Kijana aliendelea kumsihi Bi Kizee amuelekeze afanye nini ili afike mlimani, Bi Kizee akajibu masharti ya kwenda kilimani ni haya yafutayo: 1, Unapoanza safari ya kwenda mlimani kuna watu watakupigia kelele nyingi sana na kusema huyo huyo huyo huyo na jinsi unayoendelea kwenda juu mlimani, kelele zitaongezeka na kuwa nyingi zaidi, zikisema mchinje huyo huyo mchinje mkamate huyo huyo, wewe uwe makini endelea na safari yako bila kugeuka nyuma mpaka ufike. Ukifanya hivyo utafanikiwa vinginevyo, 2, ukigeuka nyuma tu utakuwa jiwe la chumvi kama unavyoona mlima huu una vichuguu vingi hao ni vijana wenzako waliogeuka jiwe. Bibi Kizee aliendelea ukifika utaweza kumpata binti, vilevile utapata dawa ya kuwaokoa vijana wenzako waliokuwa wanapanda kwaa lengo kama lako lakini wakashindwa na kugeuka jiwe. Kijana alikubali masharti na kuanza safari, alipigiwa kelele nyingi sana huyo huyo huyo mchinje huyo huyo lakini katu hakusikiliza, mpaka akafanikiwa kufika mlimani na kumpata binti, pia dawa ya kumwagia yale mawe, ambapo yaligeuka kuwa vijana waliopanda mlima awali. Hadithi hii ya Mwalimu aliifafanua na kusema; Unapotaka kujenga nchi ya Haki na isiyo na dhuluma kwa wananchi wako na wale unaowaongoza ni kazi ngumu kweli kweli, unahitaji kuwa mjasiri na kufanya kazi kwa ujasiri mkubwa bila kugeuka nyuma mpaka ufanikiwe kuijenga nchi yenye haki bila dhuluma. Mwalimu aliongezaa safari hii itakuletea maadui wengi wanaopenda kupindisha haki na dhuluma kutoka ndani na nje ya nchi. Mwalimu hakika umesema kweli na msema kweli ni mpenzi wa Mungu, mambo tunayoyaona yakitokea katika uongozi wa awamu ya tano ya Rais Dkt John Pombe Magufuli ndiyo hayo uliyoyatamka tarehe moja mwezi Mei mwaka 1981 pale Tabora. Mishale na mikuki ya maneno ya kejeli na fedheha, dhihaka na yanayofedhehesha, pamoja na kelele huyo huyo huyo, mchinje mpige mawe huyo huyo, anatupiwa Kiongozi wetu kwa kuwa tu amesimama kwenye misingi ya Haki na kuondoa dhuluma kwa wananchi wanyonge, ambao walishakata tamaa na kuona nchi imevamiwa na wapiga dili. Hali hii ya kupokea taarifa za wapiga dili kila uchweo limewachosha Watanzania na kwa kiasi kikubwa linasababisha watanzania wapenda haki, wazalendo na wale wenye maadili tangu enzi za Baba wa Taifa kustaajabu na kushangaa wanabaki wakijiuliza hivi hao wapiga dili ni watanzania au wanatoka nje ya nchi? Ukifikiri sana utadhani wana nchi nyingine wanayoitegemea na sio hii. Maneno ya Mwalimu amewahusia viongozi watakaoiongoza nchi ya Tanzania na hususan kwa Rais aliyepo madarakani Dkt, Magufuli kwa kuwa ni kiongozi aliyedhamiria kuondoa dhuluma na kuleta haki kwa wanyonge wa Tanzania. Kuondoa madhila yote ya unyonyaji wa hali yoyote ile uwe wa kiuchumi katika Maliasili zetu Raislimali za madini, Gesi, fedha za Umma, Madaraka, Ardhi, katika siasa uongozi bora na utawala unaoheshimu haki za wanyonge na watanzania kwa ujumla. Mwalimu ulisema vema wanaopenda haki ipindishwe na dhuluma ihalalishwe wapo humu humu ndani ya Tanzania wanadiriki kusaidia wapinga haki wa nje ili waweze kufanikiwa kukwamisha maendeleo ya nchi yetu. Sio jambo la kushabikia lakini lipo na wanaona fahari kabisa na kujisifu kuwa wao ndio wako kwenye mstari na kushawishi wananchi waone ni sahihi na kuungwa mkono. Jambo hili halikubaliki, na litapingwa kwa nguvu zote na wapenda maendeleo wa nchi hii, nina hakika vita hii Rais Magufuli atashinda. Suala moja la kutia moyo ni kwamba wananchi wa Tanzania waliowengi wameliona hili na kuamua kumuunga mkono. Mara tufikapo kilimani na kupata nchi ya Asali na Maziwa tutawamwagia dawa wale wote waliogeuka mawe ili warejee na kufaidi maziwa na Asali kama watanzania wengine. Mungu Ibariki Tanzania Mungu inbariki nchi yetu. Pumzika kwa Amani Mwalimu. Mwisho.

Comments

Tanzania

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

Hatua za Ugonjwa wa UKIMWI

MAITI YAOKOTWA IKIWA KWENYE MFUKO, MIKONO NA MIGUU YAFUNGWA KAMBA KWA NYUMA