Kitabu chavutia wengi


KITABU CHA SAKATA LA FEDHA HARAMU (50) KILICHOANDIKWA NA MWANDISHI / MTUNZI: INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO) kimeonekana kuwavutia wengi hasa kutokana na simulizi zake kuonekana kuwa fundisho tosha kwa maisha ya wengi. Baadhi ya watu waliokisoma wanaamini kwamba ikiwa wengi wangekuwa na tabia ya kusoma vitabu, basi huenda kuna mengi ambayo yangebadilika katika maisha yao... Sehemu mojawapo ya kitabu inasema..... Danny alibaki akimwangalia kwa macho ya hasira, akionekana kama mtu asiyekata tamaa, na kwa kweli bado alikuwa hajafikia hatua ya kukata tamaa japo maumivu makali yalizidi kumwandama katika mkono wake uliojeruhiwa na risasi. Ukumbi ulikuwa umebaki tupu! Kila mtu aliyekuwa humo alikuwa amekimbia katika kunusuru maisha yake. Halfan alikuwa akitamba huku na kule, mara akimwangalia Danny na mara akamwangalia Maftah. Alitambua fika alipaswa kuwa makini na kwamba kama atajisahau na kuanza kumhudumia Maftah, huenda huyu Danny akaibuka kama shetani na kufanya lolote linaloweza kuhatarisha usalama wao. Hivyo, papohapo alitwaa simu na kupiga kituo kikuu cha polisi, akihitaji msaada zaidi. Baada ya kuhakikisha kuwa taarifa yake imepokewa, ndipo akamrudia Maftah. ***SURA YA ISHIRINI NA TISA*** DORA alitembea taratibu akiamini kuwa si rahisi kwa mtu yeyote kumtambua kutokana na haya mabadiliko ya mavazi. Hata wafanyakazi wenzake, isingekuwa rahisi kumtambua kwa kuwa aliamini hakukuwa na yeyote aliyewahi kumwona akiwa amevaa hivyo. Alivuka mtaa mmoja, akipita kwenye uchochoro kisha akatokeza upande wa pili. Hapo akakuta kuna baa iliyochangamka sana kama ile aliyomkuta Rodgers mchana kule Makumbusho. Runinga bapa mbili kubwa zilikuwa pande mbili za baa hiyo kwa juu, hivyo hakuna aliyepata shida ya kuona kila kilichooneshwa na kusikia kila kilichosemwa. Dora aliangaza macho huku na kule na akabaini kuwa hata wateja wa hapo nao walimwangalia kwa macho yenye maswali akilini mwao. Hakuipenda hali hiyo. Akajiuliza, kwani yuko tofauti na wanadamu wengine au wateja walioko humo? Mbona kuna wanawake zaidi ya kumi katika meza tofauti wakiburudika na vinywaji vyao? Kuna tofauti gani ya wao na yeye? Lakini papohapo akajishtukia. Akili ilichangamka na akabaini kuwa huenda ni vazi lake lililowachanganya. Kumwona mwanamke aliyevaa baibui akiingia baa lilikuwa ni jambo la kushangaza kwa watu wengi. Huchukuliwa kuwa hilo ni vazi la heshima zaidi, lisilostahili kupenya ndani ya majengo kama haya! Huku kwa mbali moyo ukimdunda kwa wasiwasi wa kuja kuonwa hata na mtu asiyetaka amwone, alikwenda mwisho wa baa hiyo, kwa nyuma, ambako hakukuwa na kiti na kulikuwa na kijigiza cha wastani na pia kando yake kukiwa na uwazi ambao mtu yeyote angeweza kuutumia kwa kuondokea. Kwa jumla baa hiyo haikuwa na ubora uliostahili kiasi cha kuonekana kuwa ni sehemu bora kwa starehe. Ilikuwa ‘kiuswazi-uswazi’ zaidi. Hata hivyo, Dora hakujali usafi sana wa mazingira ya hapo, alichojali ni usalama wake na kupata kile kilichomleta. Hivyo, japo eneo hilo halikuwa na kiti wala meza, alisimama kiambazani tu akiwaangalia wote waliokuwa mbele yake. Mara mhudumu mmoja wa kiume akamfuata. “Sista mbona umejitenga sana?” mhudumu huyo alimuuliza. “Karibu kuna siti pale mbele kwenye mwanga. Huku kuna mbu wengi sana dada’angu.” “Us’jali, sikai sana.” “Ok, hiari yako. Nikuletee kiti?” “Itakuwa poa sana.” Mhudumu huyo aliondoka haraka na baada ya muda mfupi akarejea akiwa na kiti pamoja na kistuli. Alikuwa akitarajia kuwa Dora ama ataagiza chakula au ataagiza kinywaji. Mara tu Dora alipoketi, akamuuliza, “Kuna chakula gani?” “Ugali nyama choma, chipsi, supu ya ulimi, kongoro na mchemsho wa samaki wa maji baridi wa Mwanza wanaitwa sato.” “Sato?” Dora alimuuliza huku akimtazama kama asiyemwamini. “Ndiyo, sato wa Ziwa Victoria.” “Wako vizuri?” “Utawapenda dada’ngu.” “Ok, niletee, pande la kichwa na ndizi mbili. Hakikisha kuna macho yale ya samaki. Hakuna nikipendacho katika supu ya samaki kama yale macho yake!" Mhudumu huyo alipoondoka, Dora alibaki amekodoa macho kwenye skrini ya runinga. Ilikuwa ni saa mbili kamili usiku na kituo fulani kilikuwa kikiashiria kutangaza taarifa ya habari. Kwa jinsi siku hiyo ilivyokuwa ikiishia kwa matukio ya aina yake, Dora alihitaji kujua jamii au Jeshi la Polisi linajua nini na limefika wapi katika hatua zozote lilizochukua. Hivyo, aliyagandisha macho kwenye runinga akitaka asipitwe na chochote. Pesa za kampuni zimeporwa, mauaji yametokea, yeye akiwa ni mtunza fedha mkuu ametoroka hospitalini! Hizo zilikuwa ni habari nzito na ambazo kwa namna yoyote ile lazima zingepewa kipaumbele kwenye vyombo mbalimbali vikubwa vya habari. Punde taarifa ya habari ikaanza, ikizungumzia tamko la Jeshi la Polisi kuhusu Sikukuu ya Krismasi iliyokuwa mbele kiasi cha siku tano na kisha wiki moja baadaye sikukuu nyingine ya Mwaka Mpya. Chombo hicho cha habari kilimkariri Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, akiwataka wakazi wa jiji hilo kuwa watulivu katika kipindi hicho na kwamba jeshi hilo halitamvumilia mtu yeyote atakayejaribu kuleta hali ya kuondoa utulivu na amani. Pia kamanda huyo alipiga marufuku disko lililohusisha watoto, maarufu kama ‘disko toto’ na pia kuwataka wazazi kuwa makini na watoto wao, akiwatahadharisha kuwa katika vipindi vya sikukuu kubwa za kidini watoto wengi hupotea katika mazingira ya kutatanisha na wengine huenda kuogelea baharini na baadhi yao kwa kutojua kuogelea, huzama. Mwishoni mwa tamko hilo la Jeshi la Polisi lilikuwa ni kamanda huyo kuwatakia heri Watanzania wote katika sikukuu hiyo na itakayofuata wiki moja baadaye. Dora alitulia akiangalia na kusikiliza tu lakini kwa jumla taarifa hiyo pamoja na nyingine iliyofuatia, iliyohusu kauli ya serikali kuhusu kupotea kwa mnyama aliyezitawala akili Watanzania wengi na vyombo mbalimbali vya habari sanjari na viongozi wengi wa ngazi za juu serikalini, ‘faru John,’ kwake haikuwa habari ya maana. Kupotea kwa ‘faru John,’ kwake ilikuwa ni hadithi ya kawaida tu na iliyokinaisha kinywani na kukera masikioni. “Faru John…faru John… nini faru John…hata mbwa Juma wapo… kuna swala Thomas, ng’ombe Jackson…kila siku faru John faru John!” alinong’ona akionesha dhahiri kukerwa na taarifa hiyo. Akilini mwake aliamini kuwa kuna matukio makubwa, na makubwa zaidi yaliyofanywa ambayo yanaweza kuwa kero kwa Watanzania kwa kiwango kisichokadirika. Kuna kashfa mbalimbali zinazohusu madini, na umiliki wa ardhi. Akaendelea kuishambulia supu yake huku bado akisubiri kuona taarifa inayofuata. Naam, hatimaye ndipo alikisikia kile alichokuwa akikisubiri. Taarifa kuhusu tukio la kuporwa pesa za kampuni ya David Motors ilitajwa na kuzungumzwa wa kina. Kilichomtisha ni kauli kuwa Jeshi la Polisi linamsaka mtunzahazina wa kampuni hiyo, ambaye inasemekana alikuwa amelazwa hospitali lakini akatoroka katika mazingira ya kutatanisha. Taarifa hiyo ikadai pia kuwa mtu mmoja ambaye inasemekana kuwa alihusika na tukio hilo amekamatwa eneo la Kigogo baada ya kupambana na askari. Pia ikatajwa kuwa kupatikana kwa mtu huyo kunafuatia kifo cha mtu mmoja aliyegongwa gari eneo la Kinondoni wakati akivuka barabara akikimbia baada ya kumwacha mwanamke aliyekuwa akinywa naye pombe akiwa chumbani hoi. Taarifa za uchunguzi kupitia mitandao ya simu ndiyo iliyolisaidia jeshi hilo kuweza kumpata mtuhumiwa mmoja eneo la Kigogo na inasemekana zaidi ya huyo mtunzahazina pia kuna mtu mwingine aliye katika mtandao huo, anayeendelea kusakwa. Taarifa hiyo ya Polisi ilisema kuwa, kwa kuwa bado uchunguzi unaendelea hakutakuwa na taarifa nyingine ili kuepuka kuharibu kazi iliyokuwa ikiendelea, ambayo iliwapa mwanga mzuri. Dora alishtuka na akawaza ni nani huyo atayekuwa amekamatwa Kigogo? Je, na huyo atakayekuwa kagongwa gari Kinondoni ni nani? Haikumwingia akilini kuwa huenda na Rodgers akawa ametiwa mbaroni, lakini aliamini kuwa huenda mawasiliano ya simu ndiyo yaliyowaponza hao waliokamatwa hususan huyo aliyekamatwa Kigogo. Sasa alijua kuwa na yeye anasakwa! Afanye nini? Wakati watu wanajiandaa kusherehekea Krismasi kwa utulivu mwilini na akilini kisaikolojia, yeye yuko ovyo, hana raha wala amani ingawa ana mamilioni ya pesa. Mara akajiwa na akili ya kumpigia simu Rodgers. Ndiyo, aliamua kuwa atakaporudi kule chumbani kwake, jambo la kwanza kufanya ni kuitwaa simu na kumpigia Rodgers haraka. Kama atampata, atajua kuwa yeye siyo miongoni mwa waliokumbwa na kamatakamata. Alikumbuka kuwa simu yenyewe haina hata saa tatu tangu aiweke kwenye chaji, lakini kwani kuongea muda huu ni kosa la jinai kwamba simu itazima moja kwa moja eti kwa kuwa tu kakiuka kanuni ya kuichaji kwa saa sita? Hakuwa mgeni wa matumizi ya simu mpya. Alishawahi kununua simu na kuichaji kwa saa tatu au nne tu na alipokumbwa na dharura aliitoa na kuitumia. Hii kanuni ya leo hakuiona kuwa ni muhimu na ya lazima sana. Usalama wake kwanza, umuhimu wa kanuni baadaye. (KWA HISANI YA OMARY BADI) KITABU: SAKATA LA FEDHA HARAMU (50) MWANDISHI / MTUNZI: INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO) SIMU: 0659 278 693 DAR ES SALAAM

Comments

Tanzania

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

Hatua za Ugonjwa wa UKIMWI

MAITI YAOKOTWA IKIWA KWENYE MFUKO, MIKONO NA MIGUU YAFUNGWA KAMBA KWA NYUMA