MBOLEA KUTOKA NJE YA NCHINI IWE CHACHU YA KILIMO CHENYE TIJA


Jovina Bujulu-MAELEZO Hivi karibuni, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea (TFRA) imeingiza nchini mbolea yenye uzito wa tani 55,000 kwa mfumo mpya wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja bila kuwepo malipo ya ziada bandarini. Mfumo huo utasaidia kupunguza bei na kuhamasisha matumizi ya mbolea kwa wakulima wengi nchini. Uingizwaji wa mbolea hiyo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2017/18, mjini Dodoma. DKt. Tizeba alisema kuwa kuanzia msimu wa 2017/18 Serikali itaanza kuagiza mbolea kwa mfumo wa pamoja kwa kuanza kuagiza aina mbili za mbolea ambazo ni mbolea ya kupandia (DAP) na ya kukuzia (UREA), kwa kuwa ndizo zinatumika sana nchini. Alitaja sababu za kutumia mfumo huo kuwa ni pamoja na kuongeza matumizi ya mbolea nchini kwa kuhakikisha kuwa wadau wote wanapata uhakika wa upatikanaji wa mbolea kwa bei ya ushindani. Aidha, mfumo huo unawawezesha wafanyabiashara wadogo wanapata nafasi ya kuagiza mbolea na kuimarisha mtandao wa usambazaji hadi ngazi ya mkulima. Vilevile utaratibu huo unawawezesha waagizaji kununua mbolea wakati bei ikiwa ndogo na TFRA kufuatilia bei hiyo ili kuepuka mwanya wa waagizaji kuongeza bei zaidi ya ile iliyonunuliwa kwa bei ndogo. Kabla ya uamuzi wa Serikali wa kuagiza mbolea kwa kutumia mfumo huu matumizi ya mbolea hayakuwa ya kuridhisha kutokana na mbolea kuwa na bei kubwa jambo ambalo liliwafanya wakulima, hasa wadogo kushindwa kumudu bei hiyo. Hivyo baada ya Serikali kupitia tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu waelekezi wa ndani na nje ya nchi kwa kutumia uzoefu wa taasisi nyingine zinazofanya ununuzi wa bidhaa kwa pamoja,ikaamua kutumia njia ambayo inawapa wakulima unafuu wa bei wakati wa kununua mbolea hizo. Kaimu Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Lazaro Kitandu amesema kuwa mbolea iliyoletwa nchini imegharimu zaidi ya shilingi bilioni 10, ambapo wafanyabiashara wa Morocco kupitia kampuni ya OCPSA wameingiza tani 23,000 za mbolea ya kupandia (DAP) na kampuni ya Premium Agro Chem ya Tanzania wameingiza tani 32,000 za mbolea ya kukuzia (UREA). Mamlaka imehakiki vyombo vya kupimia mbolea hiyo ili iwe na viwango vinavyokidhi ikiwa ni pamoja na kusimamia ugawaji bila kuwepo uchakachuaji. Kitandu amesema kuwa Serikali imepanga kutoa mbolea hiyo kwa bei nafuu ambapo mamlaka itasimamia katika kila ngazi ili kusaidia wakulima kufikia malengo ikiwa ni pamoja na kudhibiti bei toka kule inapotoka na kuhakikisha inauzwa kulingana na bei ya soko la dunia. Kuhusu namna mbolea itakavyowafikia wakulima, Kitandu alisema kuwa mbolea hiyo inatarajiwa kusambazwa zaidi kwa kutumia usafiri wa treni ili kupunguza gharama za usafirishaji. Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba alisema kuwa bei elekezi ya mbolea itatangazwa kupitia vyombo vya habari na kutoa onyo kwa mawakala kujipangia bei kwa kuuza mbolea nje ya bei elekezi na kwamba ikibainika hatua za kisheria kama vile kunyang’anywa leseni,kufungiwa, faini au hatua zote kwa pamoja zitachukuliwa. Aidha, alisema kuwa bei hizo zitasimamiwa katika kila ngazi na kuzitaka mamlaka husika kuanzia Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na vijiji kuhakikisha kuwa bei elekezi itakayotolewa na Serikali inafuatwa kwa sababu mamlaka ya mbolea pekee haiwezi kuwa na wasimamizi kila mahali. “Ununuzi wa mbolea kwa pamoja utasaidia kudhibiti bei, iwapo iwapo kutajitokeza ongezeko lisilokuwa na sababu (soko holela), kwa kuwa bei itatangazwa kwa kuzingatia bei halisi ya mbolea na gharama halisi za usafirishaji ikiwemo kiwango stahiki cha faida kwa mfanyabiashara” alisema Kitandu. Utaratibu huu utawainua wakulima katika uzalishaji wa mazao kwa kuwa watakuwa na uwezo wa kununua mbolea kwa bei nafuu pia wakati huo huo watakuwa na uhakika mbolea hiyo ina viwango vinavyokidhi kwa kuwa inaingizwa nchini na kusambazwa na mamlaka yenye dhamana. Pamoja na uhakika wa mbolea yenye bei nafuu na yenye viwango stahiki, wakulima wanatarajiwa kupata faida ya kupatiwa mafunzo kuhusu matumizi ya mbolea hizo kutoka kwa wataalamu wa mamlaka ya udhibiti, hivyo kuwa na matumizi sahihi ya mbolea. Ikiwa wakulima watatumia nafasi hii vizuri, sekta ya kilimo nchini inategemewa kuwa na manufaa wakulima na taifa kwa ujumla. Mfumo huo utawawezesha wafanyabiashara wadogo kukua na kushiriki katika biashara ya mbolea na kuimarisha mtandao wa usambazaji kuanzia ngazi ya wakulima wakubwa hadi kwa mkulima mdogo. Serikali inatarajia matokeo chanya katika kupunguza bei ya mbolea kwa wakulima itakayosaidia kuongeza matumizi ya mbolea na uzalishaji wenye tija ambao utachochea na kuimarisha uchumi wa viwanda. MWISHO.

Comments

Tanzania

TAARIFA MBAYA KWA WAVUTAJI WA SIGARA, TUMBAKU

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

MADAI YA WAFANYAKAZI YASABABISHA VIFAA VYA UJENZI VYA KAMPUNI YA  CEYTUN KUZUIWA UWANJA WA NDEGE TABORA.