SERIKALI KUENDELEZA MAHUSIANO NA WASHIRIKA WA MAENDELEO.


Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na kujenga mahusiano mazuri na Washirika wa Maendeleo ili kuwezesha kufanikisha azma ya kushirikiana katika kuleta maendeleo nchini. Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa uzinduzi wa Awamu ya pili ya Mradi wa kulijengea uwezo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo mjini Dodoma. “Kwa nia ya kuhakikisha miradi kama hii inayofadhiliwa na Washirika wa Maendeleo inaleta tija, Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na kujenga mahusiano mazuri kwa lengo la kufanikisha azma katika kuleta maendeleo,” alisema Majaliwa. Aidha Majaliwa ameongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi kama hii ili kuhakikisha masharti na vigezo mbalimbali vilivyowekwa vinazingatiwa wakati wa utekelezaji wake. Mbali na hayo waziri Mkuu amesema kuwa, Serikali inatambua umuhimu wa kushirikiana na Bunge ikiwa ni pamoja na kuendelea kulijengea uwezo Bunge hilo ili liweze kuisaidia Serikali katika kuleta maendeleo na kupunguza umaskini. Kwa upande wake Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilillah amesema kuwa Mradi huo ni matokeo ya mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Bunge la Tanzania na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). “Lengo la mradi ni kuongeza uwezo kwa wabunge, watumishi na wananchi kwa ujumla ambapo Mradi umejikita katika masuala ya Utungaji wa Sheria, Usimamizi wa Bajeti ya Serikali pamoja na ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za kibunge” ameongeza  Dkt. kashilila   Nae Balozi wa Ireland nchini Tanzania Paul Sherlock amesema Mradi huo utawezesha Bunge kuimarisha wabunge na watumishi wa bunge kupata elimu na ujuzi katika maeneo yao ya kazi. Mradi huo umefadhiliwa na Washirika wa Maendeleo wakiwemo UNDP, Serikali ya Ireland, Serikali ya Uingereza kupitia Shirika lake la Maendeleo la DFID, Serikali ya Dermark pamoja na Serikali ya Sweden.

Comments

Tanzania

TAARIFA MBAYA KWA WAVUTAJI WA SIGARA, TUMBAKU

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

MADAI YA WAFANYAKAZI YASABABISHA VIFAA VYA UJENZI VYA KAMPUNI YA  CEYTUN KUZUIWA UWANJA WA NDEGE TABORA.