Serikali Yawataka Wageni Wanaoingia Nchini Kufuata Sheria.


Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma. Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imewataka wageni wanaoingia nchini kufuata sheria za nchi na imewaonya wale wanaojihususha na usafirishaji au kuwaficha wahamiaji haramu kuacha tabia hiyo mara moja. Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni, mjini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mwigulu Nchemba alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Zubeda Sakuru juu ya kauli ya Serikali kufuatia ongezeko la wahamiaji haramu nchini. “Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji imekuwa ikiendeleza mapambano dhidi ya wahamiaji haramu na kuwachukulia hatua za kisheria ili kuhakikisha nchini yetu inakuwa salama,” alifafanua Mwigulu Nchemba. Ameendelea kusema kuwa katika kupambana na wahamiaji haramu, Idara ya Uhamiaji imeendelea kuchukua juhudi za kuendesha doria na misako mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama. Aidha, Waziri Mwigulu amesema kuwa kwa mwaka 2016/17 jumla ya watuhumiwa 9,581 na wahamiaji haramu walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali kisheria. Hata hivyo Serikali inaendelea kuimarisha vitendea kazi kama vile magari ili kuweza kudhibiti mipaka, kutoa elimu kwa Umma juu ya madhara ya kuhifadhi wahamiaji haramu na kupambana na mtandao wa wasafirishaji haramu wa binadamu. Vile vile amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2016/17 jumla ya wasafirishaji haramu wa binadamu 28 wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani. Pia magari Sita yalithibitika kuhusika yalikamatwa na kuataifishwa kwa amri ya Mahakama.                                                                                                                        Nia ya Serikali ni kuendelea kuimarisha ulinzi wa mipaka na kutokomeza uhamaaji haramu nchini.

Comments

Tanzania

TAARIFA MBAYA KWA WAVUTAJI WA SIGARA, TUMBAKU

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

MADAI YA WAFANYAKAZI YASABABISHA VIFAA VYA UJENZI VYA KAMPUNI YA  CEYTUN KUZUIWA UWANJA WA NDEGE TABORA.