Tanzania kuandaa mkutano wa kimataifa wa usafiri endelevu mwakani


Tanzania kuandaa mkutano wa kimataifa wa usafiri endelevu mwakani Na Mwandishi wetu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Mhandisi Ronald Lwakatare amesema kuwa Serikali ya Tanzania imepewa heshima ya kuandaa mkutano wa kimataifa wa usafirishaji endelevu utakaofanyika katika jiji la Dar es salaam kati ya mwezi wa sita hadi wa saba mwaka 2018. Heshima hiyo imetokana na Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) uliopo katika jiji la Dar es salaam kutangazwa kushinda tuzo ya usafirishaji endelevu katika mkutano wa usafirishaji endelevu uliofanyika mnamo mwezi mei, 2017 katika mji wa Santiago nchini Chile na hivyo kuliwezesha jiji la Dar es salaam kushinda tuzo hiyo kwa mwaka 2018. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana wakati akielezea mafanikio na changamoto mbalimbali zilizotokana na utekelezaji wa mradi huo kwa kipindi cha mwaka mmoja, Mhandisi Lwakatare ameeleza kuwa sasa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka upo katika maandalizi kwa ajili ya mkutano huo mkubwa wa kimataifa. “Katika heshima hiyo, mkutano ujao, ambao kama uliofanyika mwaka huu, ambao ulitutangaza sisi kama washindi, sisi tumepewa heshima ya kuwa wenyeji wa mkutano huo ambao utafanyika katika jiji la Dar es salaam mwakani,” alisema. Mhandisi Lwakatare alieleza kuwa mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na wageni kutoka nchi nyingi kutoka Bara la Afrika na kote duniani. “Kutakuwa na mada mbalimbali zitakazotolewa kuhusiana na usafiri wa umma, nasi tumefurahi kupata heshima hiyo ya kuwa mwenyeji wa mkutano huo,” alifafanua. Mhandisi Lwakatare aliongeza kuwa mkutano huo unatarajiwa kufanyika kwa muda wa siku mbili au tatu kati ya mwezi juni au julai mwaka 2018. Wakati huo huo, Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka unatarajiwa kukabidhiwa tuzo ya usafirishaji endelevu kwa mwaka 2018 katika hafla inayotarajiwa kufanyika mwezi januari mwakani katika jiji la Washington nchini Marekani. Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka ni Taasisi ya Serikali iliyo chini ya Ofisi ya Rais- TAMISEMI na inatekeleza Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka kwa njia ya ubia na kampuni binafsi ya UDART. Mradi huo ulianza kutoa huduma ya mabasi wakati wa mpito kuanzia tarehe 10 Mei, 2016.

Comments

Tanzania

TAARIFA MBAYA KWA WAVUTAJI WA SIGARA, TUMBAKU

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

MADAI YA WAFANYAKAZI YASABABISHA VIFAA VYA UJENZI VYA KAMPUNI YA  CEYTUN KUZUIWA UWANJA WA NDEGE TABORA.