WANANCHI WA MKOA WA KASKAZINI UNGUJA WAHIMIZWA KUJIUNGA NA JUMUIYA YAO.


Na Miza Kona, MAELEZO MAKAMU wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, ameitaka Jumuiya ya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kuzidisha mshikamano  ili kuweza kubadilika kielimu na kuleta maendeleo mazuri mkoani humo. Balozi Seif ameyasema hayo katika ukumbi wa  zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni mjini Zanzibar katika mkutano wa Jumuiya hiyo. Alisema vijana wengi wa mkoa huo wanakosa kuingia katika ushindani wa soko la ajira kutokana na kukosa sifa zinazohitajika. Balozi Seif alisema jumuiya inaweza kuleta mafanikio makubwa  kwa kushirikana  pamoja na kuzidisha mshikamano katika dhamira ya kuibadilisha jamii ya mkoa huo kielimu. Alifahamisha kuwa elimu ndio silaha pekee inayoweza kuwakomboa vijana na kuwawezesha kukubalika katika ajira mbalimbali na hivyo kuondokana na umasikini. “Ni wakati sasa wa kubadilika kwa kuwekeza katika elimu ya watoto wetu ili kuwainua vijana na kuwawezesha kuhimili ushindani kwa kuwa na sifa zitakazoweza kuajiriwa au kujiajiri,” alifahamisha Balozi Seif. Alieleza vijana wengi wa mkoa huo hawana mwamko wa kusoma, jambo linachangia mkoa wa Kaskazini kuwa nyuma kielimu na kimaendeleo ikilinganishwa na mikoa mingine nchini. Amehimiza kuwepo ushirikiano wa pamoja baina ya viongozi na wana jumuiya katika kuishajiisha jamii ili iweze kubadilika kiuchumi na kuacha kuingiza itikadi za siasa katika suala la kuleta maendeleo. Balozi Seif alisema jumuiya ina nia ya kuimarisha umoja na kuleta maendeleo katika mkoa huo. Aidha Makamu wa Pili  wa Rais amewasisitiza viongozi wa majimbo na serikali katika mkoa huo kudumisha ushirikiano na kuwasaidia vijana wasio na uwezo wa kujikimu kwa kuwapa msukumo wa kimaendeleo pamoja na kuishajiisha jamii kujiunga jumuiya hiyo. Jumuiya Maendeleo ya Mkoa wa Kaskazini Unguja (NUDO), imeasisiwa mwezi Aprili 2016, na sasa ina zaidi ya wanachama zaidi ya 1000. Lengo la kuanzishwa kwake ni kuendeleza, kuwezesha na kuijengea uwezo jamii ya mkoa huo katika kuinua ustawi wake kiuchumi, kijamii na mazingira.

Comments

Tanzania

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, MHE. UMMY A. MWALIMU (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA 2018/2019

Hatua za Ugonjwa wa UKIMWI

MAITI YAOKOTWA IKIWA KWENYE MFUKO, MIKONO NA MIGUU YAFUNGWA KAMBA KWA NYUMA